'
Sunday, July 21, 2013
SIMBA HOI KWA URA
Mshambuliaji wa Simba, Betram Mwombeki akishangilia kwa staili ya aina yake baada ya kuifungia Simba bao la kuongoza katika mechi ya kimatifa ya kirafiki dhidi ya URA ya Uganda iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. URA ilishinda 2-1. (Picha na Bin Zubeiry)
SIMBA jana ilipigwa mweleka wa mabao 2-1 na URA ya Uganda katika mechi ya kirafiki ya kimataifa ya soka iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pamoja na kupokea kichapo hicho, vijana wa Simba, ambao wengi ni wapya walionyesha kiwango cha juu cha soka, hasa kipindi cha kwanza na kuwafanya washangiliwe na mashabiki wao.
Iliwachukua Simba dakika saba kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wake mpya, Betram Mwombeki kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Ramadhani Singano 'Messi'. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.
URA ilisawazisha dakika ya 60 kwa bao lililofungwa na Lusimba Yayi baada ya mabeki wa Simba kuzubaa kuokoa shambulizi kwenye lango lao.
Simba ilipata pigo dakika ya 65 baada ya Mwombeki kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga kiwiko beki, Jonathan Mugaba.
Pengo hilo liliiwezesha URA kupata bao la pili dakika ya 75 lililofungwa na Yayi baada ya kupokea pasi kutoka kwa Derick Walulya, aliyepanda mbele kusaidia mashambulizi.
URA inatarajiwa kushuka tena dimbani leo kucheza na Yanga kwenye uwanja huo.
Simba SC; Abbel Dhaira, Nassor Masoud ‘Chollo’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Rahim Juma/Sino Augustino, Samuel Ssenkoom, Jonas Mkude, Ramadhani Singano/Miraj Adam, William Lucian, Betram Mombeki, Zahor Pazi/Twaha Ibrahim na Marcel Boniventura.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment