KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 14, 2013

AZAM TV YAELEZA ITAKAVYOONYESHA MECHI ZA LIGI KUU



UONGOZI wa Azam TV umetoa taarifa ya ufafanua kuhusu utaratibu utakaotumiwa na kituo hicho katika kuonyesha laivu baadhi ya mechi za michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Azam TV imetoa ufafanuzi huo kufuatia wadau wengi wa soka nchini kuhoji zilipo ofisi za kituo hicho na iwapo kimeshapatiwa leseni ya kufanyakazi nchini.

Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam juzi, Ofisa wa Azam TV, Patrick Mwakamele alisema, kituo chake hakihitaji kuwa na mitambo ili kiweze kufanyakazi zake.

Mwakamele alisema kutokana na mabadiliko ya teknolojia duniani, Azam TV itafanya kazi zake kwa kunua masafa kwenye 'satelaiti' kama vinavyofanya vituo vingine vya televisheni kama vile Dstv.

Alisema mfumo huo ni mgeni kwa watanzania kwa sababu wamezoea kuviona vituo vya televisheni vikiwa na mitambo yake ya kufanyiakazi.

Kwa mujibu wa Mwakamele, uonyeshaji wa mechi za ligi hiyo pia unaweza kufanyika kupitia vituo vingine vya televisheni kama vile Star TV na Channel Ten kwa makubaliano maalumu ili kuwawezesha mashabiki wengi zaidi kuzishuhudia.

"Baada ya mkataba kati yetu na kamati ya ligi kuridhiwa, tutakuwa na chaneli yetu ya Azam TV kwenye satelaiti na tunatarajia kuanza kuuza ving'amuzi vyetu kabla ya kuanza kwa ligi,"alisema.

Akifafanua, Mwakamele alisema upatikanaji wa ving'amuzi hiyo hautakuwa na matatizo kwa sababu Azam ina mtandao nchi nzima, hivyo vitapatikana kwa urahisi.

Ofisa huyo wa Azam TV alisema ving'amuzi hivyo vitakuwa na uwezo wa kurekodi mechi na kuongeza kuwa, kila timu itakuwa ikipatiwa CD ya mechi zake kwa ajili ya kumbukumbu.

Hata hivyo, Mwakamele alisema tayari maandalizi ya ujenzi wa studio za Azam TV 
yameshaanza na kuongeza kuwa, inatarajiwa kujengwa katika moja ya maeneo ya barabara ya Mandela, Dar es Salaam.

Mwakamele ametoa mwito kwa klabu za ligi kuu, kuunga mkono mkataba huo wa Azam ili timu zao ziweze kuonekana duniani na wachezaji kupata soko la kucheza soka ya kulipwa nje ya nchi.

"Tunapaswa tuutangaze mpira wetu kimataifa, tukuze soka yetu,"alisema.

1 comment:

  1. Ninawatakia kila la kheri katika biashara hii. Ninaamini mnajua kuwa watanzania tunataka nini katika suala la michezo kazi ni kwenu. Mtaji wa kuwashinda DSTV kwa tanzania mnao fanyeni kazi.

    ReplyDelete