KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 1, 2013

POLISI WAMVUA NGUO MADEE AIRPORT J'BURG


MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Madee wa kundi la Tip Top Connections amenusurika kukamatwa nchini Afrika Kusini kwa tuhuma za kuingiza dawa za kulevya nchini humo.

Madee alipatwa na mkasa huo mwanzoni mwa wiki hii baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa mjini Johannesburg.

Akihojiwa na mtandao wa Millardayo jana, Madee alisema polisi wa Afrika Kusini walimpekua kwa saa kadhaa uwanjani hapo wakiwa na wasiwasi huenda alibeba dawa hizo.

Madee alisema alikutwa na mkasa huo, kufuatia uzito wa tukio lililowakuta wasanii wawili wa Tanzania, Agnes Jerard 'Masogange' na Melisa Edward walionaswa nchini humo mwezi huu wakituhumiwa kuingiza dawa za kulevya zenye thamani ya sh. bilioni 6.8.

"Kwa kawaida, huwa kuna utaratibu wa kukaguliwa hati ya kusafiria na ukaguzi mwingine, ambao hufanywa kwa kutumia mitambo maalumu kwa kila abiria anayeingia Afrika Kusini, lakini mimi nilikaguliwa kwa karibu dakika 60,"alisema.

Alisema askari waliokuwepo uwanjani hapo waliamua kutumia muda mrefu kumpekua baada ya kueleza kwamba anatoka Tanzania.

"Kuna wazungu wawili wenye sare tofauti za polisi walianza kunisachi mpaka kufikia hatua ya kuniambia nivue fulana na kubakiwa na nguo nyepesi ya ndani. Wakati huo, abiria wote niliosafiri nao walisharuhusiwa,"alisema.

Alisema yeye na abiria mwingine raia wa Zimbabwe ndio waliokaguliwa kwa muda mrefu. Hata hivyo, alisema raia huyo wa Zimbabwe aliruhusiwa baada ya kukaguliwa kwa dakika 10 na hakuambiwa avue nguo.

Kwa mujibu wa Madee, sehemu aliyoambiwa avue nguo haikuwa kwenye chumba maalumu, bali kwenye foleni waliposimama abiria wenzake na kwamba alizibwa kwa kioo chenye urefu wa usawa wa tumbo kushuka chini.

"Muda wote walipokuwa wakinikagua, jamaa walikuwa wakinong'onezana mara kwa mara. Sielewi walikuwa wakielezana kitu gani,"alisema Madee.

Msanii huyo alisema askari hao walilazimika kumwomba radhi baada ya kumaliza ukaguzi wao na kumweka uwanjani hapo kwa saa moja, ikiwa ni pamoja na kulivuruga begi lake la nguo.

No comments:

Post a Comment