KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 7, 2013

MINZIRO: YANGA HAINA MCHEZAJI NYOTA



KOCHA Msaidizi wa Yanga, Fred Felix Minziro amesema timu hiyo haina mchezaji nyota, anayepaswa kujiona bora kuliko wenzake.

Minziro amesema viwango vya wachezaji wote waliosajiliwa msimu huu vinalingana na kila mmoja anapaswa kupigania namba ili awemo kwenye kikosi cha kwanza.

"Wachezaji wote waliosajiliwa na Yanga wapo sawa, hakuna aliye bora kuliko wengine,"alisema kocha huyo.

Kutokana na ubora wa wachezaji wa timu hiyo, Minziro amesema kila mchezaji anayepangwa katika mechi, amekuwa akionyesha uwezo wa hali ya juu kisoka.

Minziro alisema anafurahi kuona kuwa, kikosi hicho kimekamilika katika kila idara ikiwa ni pamoja na kuwa na wachezaji zaidi ya wawili katika kila nafasi.

Katika mechi za kirafiki ilizocheza hivi karibuni, Yanga ilitoka sare ya mabao 2-2 na URA ya Uganda kabla ya kuichapa Mtibwa Sugar ya Morogoro mabao 3-1.

Kocha huyo alisema kutokana na kikosi chao kufanya usajili mzuri na kukamilika katika kila idara, wana uhakika mkubwa wa kutetea taji lao walilolitwaa msimu uliopita.

Aliwaonya wachezaji wake kuwa, yeyote atakayezembea katika msimu ujao wa ligi, ataachwa wakati wa usajili wa dirisha dogo na kusajiliwa wachezaji wengine wapya.

Yanga inatarajiwa kuanza msimu ujao wa ligi kwa kucheza mechi ya kuwania Ngao ya Jamii dhidi ya washindi wa pili wa mwaka jana, Azam. Mechi hiyo itapigwa Agosti 17 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment