KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, August 23, 2013

KASEJA: MIMI SI MCHAWI, SIJAWAHI KUIHUJUMU SIMBA


KIPA wa zamani wa klabu ya Simba, Juma Kaseja amesema tangu alipoanza kuichezea timu hiyo miaka tisa iliyopita, hakuwahi kujihusisha na masuala ya ushirikina au kuihujumu ifungwe na timu pinzani.

Kaseja amesema kucheza soka ndio kazi yake, hivyo isingekuwa rahisi kutumiwa na mtu yeyote kuihujumu Simba kwa maslahi yake binafsi.

"Uchawi? Sijawahi kujihusisha nao kabisa japokuwa Kaseja ndiye mtuhumiwa mkubwa. Tatizo ni kwamba wengi wanamjua Kaseja, hawamjui Juma," alisema Kaseja alipohojiwa katika kipindi cha Mkasi kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha East Africa mwanzoni mwa wiki hii.

"Mwenyezi Mungu amenijalia kipaji cha kucheza soka. Tangu nilipokuwa sekondari ya Makongo, nilikuwa kipa namba moja, kwa nini isiwe Simba au Taifa Stars," alisema Kaseja, ambaye pia amewahi kuzidakia timu za Yanga na Moro United.

Kipa huyo aliyeachwa na Simba katika usajili wa msimu ujao amesema, katika kipindi chote alichoichezea timu hiyo, hakuwahi kutumiwa na kiongozi yeyote ama mfadhili kuihujumu ili ifungwe.

Alisema asingekuwa tayari kucheza chini ya kiwango ili kuihujumu Simba kwa vile angefanya hivyo, angejishushia hadhi yake kisoka na asingeweza kudumu kwenye klabu hiyo kwa miaka yote tisa.

Kaseja alisema hajawahi kuhongwa fedha ili aihujumu timu yake na kwamba ugomvi wa viongozi hauwezi kumshawishi acheze chini ya kiwango kwa lengo la kuunga mkono upande mmoja.

"Mimi ni mchezaji, sitaki kujua malumbano, kazi yangu ni kucheza soka. Watu wasingemjua Kaseja kama ningejihusisha na mambo hayo. Hayo ni maneno ya kawaida tu katika soka,"alisema kipa huyo, ambaye pia ameichezea Taifa Stars kwa zaidi ya miaka saba.



Kaseja amekiri kuwa, nafasi ya kipa ni nyeti katika timu ya soka na kwamba anapofanya makosa, anafungwa kirahisi, lakini kosa hilo hilo linapofanywa na beki, kipa anaweza akaokoa.

Akizungumzia kuachwa kwake na Simba kwenye usajili wa msimu huu, Kaseja alisema kulitokana na mkataba wake kumalizika na si kweli kwamba aliachwa kwa makusudi.

Alisema baada ya mkataba wake kumalizika, yeye na viongozi wa Simba walishindwa kuelewana kuhusu mkataba mpya na ndio sababu aliamua kuachana nayo na kutafuta timu nyingine.

"Mpira ni kazi, mkataba umekwisha, hakuna maelewano, inawezekana mmoja kati yenu hakuridhika, basi mnaachana,"alisema Kaseja.

Aliongeza:" Simba si mali ya mtu, ni ya watu wengi. Nawapenda sana viongozi, wanachama na mashabiki wa Simba kwa sababu nimeishi nao kwa miaka mingi. Kuna kitu wao walikipata kutoka kwangu na mimi nimefaidika. Tumeachana kwa heri."

Kaseja alisema inasikitisha kuona kuwa, viongozi wa soka nchini hawapendi kuona mchezaji akicheza soka kwa miaka mingi katika timu moja kwa hofu kwamba atajua siri nyingi na pengine kuwatia maneno wachezaji wapya.

"Wenzetu Ulaya, mchezaji anapocheza soka kwa miaka mingi katika klabu moja, anapewa heshima kubwa. Hapa kwetu ni tofauti. Ukicheza soka kwa miaka mingi, unaitwa mzee,"alisema.

Kaseja alikanusha madai kuwa, hakuwa akipata namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Taifa Stars, ilipokuwa chini ya Kocha Marcio Maximo kwa sababu alifurahia ilipofungwa idadi kubwa ya mabao na Senegal katika michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika za 2008.

"Si kweli kwamba nilicheka kwa lengo la kufurahia kipigo kile. Hayo yalikuwa maneno ya watu tu. Mimi ni mchezaji, siwezi kufurahia kitu kama hicho ndio sababu niliamua kukaa kimya tu,"alisema.

"Inawezekana kuna watu walimtia maneno ya uongo kocha ili nionekane mbaya, lakini nisingeweza kufanya kitu kama hicho,"aliongeza.

Alisema alianza kuichezea Taifa Stars tangu wachezaji walipokuwa wakilipwa posho ya sh. 1,500 hadi sasa wanapolipwa posho ya sh. 50,000 na kwamba amekuwa akiichezea kwa mapenzi yake yote na ushirikiano mkubwa na wachezaji wenzake.

Kaseja alisema katika klabu zote alizowahi kuzichezea, ikiwemo Yanga, hakuna anakoweza kujutia kwa vile zinafanana kwa kila hali. Alisema hakuna tofauti yoyote kwa mchezaji kuichezea Yanga au Simba.

Kipa huyo alisema ameshindwa kujiunga na FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kutokana na kushindwa kuelewana na viongozi wake kuhusu mkataba.

Alisema alishafikia makubaliano ya awali na wakala wa klabu hiyo, lakini lilipokuja suala la mkataba, ndipo mambo yalipokwenda mrama.

Kwa mujibu wa Kaseja, awali lengo la FC Lupopo lilikuwa ni kumsajili kipa namba moja wa Mtibwa Sugar, lakini viongozi wake walishindwa kuelewana kuhusu malipo ya ada ya uhamisho na kiwango cha mshahara wa mchezaji huyo.

"Walipoona hivyo na baada ya kusikia habari zangu kwamba sina timu, ndipo waliponifuata mimi kwa kujua kwamba kusingekuwa na malipo ya ada ya uhamisho, lakini tumeshindwa kuelewana kuhusu mkataba,"alisema kipa huyo.

Kipa huyo mahiri alisema ni vigumu kutabiri timu ipi itatwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu kwa vile timu nyingi zimefanya maandalizi mazuri. Alisema japokuwa watu wengi wanazipa nafasi Simba na Yanga, lakini Azam inaweza kuonyesha maajabu kutokana na kuwekeza fedha nyingi katika mchezo huo.

Kaseja alisema wachezaji wengi wa Tanzania wanashindwa kucheza soka kwa miaka mingi kutokana na kubweteka baada ya kupata sifa. Alisema vyombo vya habari vimekuwa vikichangia kuua vipaji vya wachezaji kutokana na kuwapa sifa wasizostahili.

Kipa huyo alisema pia kuwa, hajutii kukosa nafasi ya kwenda kucheza soka ya kulipwa nje ya nchi, hasa barani Ulaya kwa sababu, kimaumbile, makocha wa Ulaya hupenda zaidi kuwapa nafasi hiyo makipa warefu.

"Inaniuma sana kuona nimecheza soka kwa miaka mingi hapa nyumbani. Nilitamani ninapoitwa Taifa Stars, ningekuwa natokea nje ya nchi. Lakini pengine Mungu hakuwa ameniandikia bahati hiyo. Pengine aliniandikia nipate riziki yangu hapahapa nyumbani,"alisema.

Kaseja alisema pia kuwa, hajawahi kutumia dawa za kuongeza nguvu katika soka ama kuvuta bangi. Alisema kwake, vitu hivyo viwili ni mwiko kwa vile anaamini kipaji alichopewa na Mungu kinatosha na hahitaji kitu kingine cha ziada.

Je, nini malengo ya Kaseja baada ya kustaafu soka?

"Nitakapostaafu soka, nimepanga kuwa mfanyabiashara. Mazingira ya soka ya Tanzania ni mazito na ndiyo yamenifanya nifikie uamuzi huo mapema. Sitapenda kujihusisha tena na soka,"alisema.

No comments:

Post a Comment