'
Wednesday, August 14, 2013
RAY C: MPENZI WANGU ALINIRUBUNI NIKAWA 'TEJA'
MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Rehema Chalamila amesema Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyeokoa maisha yake baada ya kumshauri akapate tiba ya
dawa za kulevya.
Rehema, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Ray C amesema, isingekuwa ushauri huo wa Rais Kikwete, huenda hali ingekuwa mbaya zaidi kwake na pengine angeweza kupoteza maisha.
Ray C alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi maalumu cha televisheni kilichorushwa hewani na kituo cha Clouds TV.
"Rais Kikwete alijitokeza, akanieleza nimesikia habari zako, usihangaike, tunazo dawa, tiba inatolewa Muhimbili na Mwananyamala,"alisema Ray C, ambaye alikuwa mwathirika wa dawa hizo kwa zaidi ya miaka mitatu.
Msanii huyo alisema awali alitibiwa katika hospitali ya Hydom ya mkoani Arusha, ambako alikutana na waathirika wengi wa dawa za kulevya, lakini hakuweza kupata nafuu.
Ray C alisema alianza kupata tiba hiyo miezi tisa iliyopita katika hospitali za Muhimbili na Mwananyama na anamshukuru Mungu kwamba kwa sasa hali yake inaendelea vizuri.
"Si unaona jinsi nilivyokuwa tipwatipwa, mwili umefura tofauti na nilivyokuwa miaka michache iliyopita,"alisema msanii huyo aliyewahi kutamba kwa vibao vyake mbalimbali kikiwemo Umenikataa bila sababu.
Akisimulia jinsi alivyojiingiza katika janga hilo, Ray C alisema ni kutokana na ushawishi alioupata kutoka kwa mpenzi wake, ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake. Alisema mpenzi wake huyo alimshawishi kutumia dawa hizo bila kujua athari zake.
"Aliponishawishi nianze kutumia, sikuelewa. Baadaye aliponiambia, nilichukia sana, lakini nilishachelewa,"alisema Ray C, ambaye aliwahi kuwa mtangazaji wa kituo cha televisheni cha East Africa.
Baada ya kubaini tatizo lililokuwa likimkabili lilikuwa kubwa, Ray C alisema alilazimika kuachana na mpenzi wake huyo na kuanza kutafuta tiba.
"Nilimpenda kwa moyo wangu wote, lakini niliamua kuachana naye kabisa. Nikasema nimtoe huyu mtu aliyeniletea balaa hili. Nilimpenda sana, lakini niliamua kumuacha aende kwa sababu ndiye aliyeniletea balaa lote hili,"alisema.
"Nikasema vyovyote iwavyo, naomba Mungu anisaidie. Nampenda huyu kijana, lakini hayuko sawa, sio kwa ajili yangu. Tulitengana 2010,"aliongeza.
Kwa mujibu wa Ray C, baada ya kutengana na mpenzi wake huyo na kubaki mwenyewe, alijaribu kupambana na ugonjwa huo, lakini haikuwa kazi rahisi.
Ray C alisema kutokana na kuathiriwa na dawa hizo, alianza kuwa mvivu wa kufanya maonyesho ya muziki, mwili ulikuwa ukimuuma na kwamba alikuwa kama mtumwa kwa vile asipotumia, alikuwa kama chizi na mgonjwa.
"Nilikuwa nikijiuliza maswali mengi sana. Mbona nimekuwa hivi? Mbona zamani nilikuwa hodari wa kazi? Nilikuwa na uwezo wa kufanya maonyesho kati ya 10 na 20 kwa mwezi, lakini sasa hata shoo moja inanitia uvivu,"alisema.
"Nilikuwa natumia kati ya shilingi milioni mbili hadi 10 kwa ajili ya kununua dawa za kulevya. Sio kwa siku moja, kwa vipindi tofauti. Biashara zote zilisimama. Mama akaanza kunishangaa. Mbona huyu siye Rehema ninayemfahamu? Nimesafiri zaidi ya nchi 20. Bidii, baraka zote nilizopewa na Mungu zimekwenda,"alisema msanii huyo akiwa katika hali ya masikitiko.
"Nikamuomba Mungu anirudishie ile bidii. Kwa hiyo nilichofanya baada ya kuachana naye, nikasema hebu nitoke nje ya nchi nikajifikirie kwanza nini kimetokea, nina tatizo gani? Hilo tatizo nimeletewa, lakini huyo mtu keshatoka, nami nitatokaje?" alisema.
Katika kuhangaika kwake kutafuta tiba, Ray C alisema aliamua kwenda nchini Kenya, lakini hakuweza kupata tiba nzuri ndio sababu akaamua kurejea nchini.
"Nikaenda Nairobi, nimekaa nikitafuta hospitali, nikasema siwezi kufanya hivi peke yangu. Napaswa kwenda nyumbani. Mama yangu yupo pale na anafahamu kila kitu. Nilishamwambia mama kwamba nina tatizo hili na lile. Akalia sana, akaomba sana. Nilishapelekwa sana kanisani, nilishafanyiwa kila kitu, lakini nilitakiwa mimi mwenyewe niamue kwamba, inatosha na nipo tayari,"alisema msanii huyo mwenye sauti yenye mvuto.
Akiwa Nairobi, Ray C alisema alipata fedha nyingi kwa kufanya maonyesho, lakini ziliishia kwenye matumizi ya dawa za kulevya. Alisema kila alichokipata, kilikwenda kwenye starehe hiyo, ambayo haikuwa na mbele wala nyuma.
"Nikipata milioni mbili hadi 10, yote inakwisha kwa sababu nilishakuwa mwathirika. Vitu vyangu vyote vilisimama. Nikawa nafanyakazi kama mtumwa,"alisema.
"Kuna wakati nilikuwa najishangaa na kujihisi kama siye mimi Ray C wa zamani. Huenda kuna mzimu uliokuwa umeingia mwilini mwangu. Mimi mwenyewe, ambaye najijua, nikasema hii si sura yangu, sura yangu ni ile ya mwanamke mchapakazi, kuhangaika kutafuta pesa, hii sura yangu ya sasa hivi sio, kama nimewekewa mzimu hivi usoni niwe mwathirika wa dawa za kulevya hadi nife,"alisema.
"Nikawa mtu wa kukaa nyumbani kusubiri waniletee nivute, imekwisha, siku inayofuata ni hivyo hivyo, ndivyo nilivyokuwa."alisema.
Ray C amekiri kuwa, hali kwa sasa hapa nchini ni mbaya kutokana na wasanii wengi kujiingiza katika janja hilo.
"Sitaki kujua wameingiaje, lakini najua kama mimi nilivyoingizwa na wao wameingizwa hivyo. Kwamba msanii anaimba tu pale, anapata milioni tano, yaani msanii hana kazi, anapiga tu yoyoyo keshapata pesa, kwa hiyo pesa zao sio za mwisho wa mwezi, saa moja tu kaimba, keshapata pesa. Kwa hiyo wanafuatwa na kuingizwa ili wakishakuwa waathirika, pesa zote wanazopata wazipate wao,"alisema.
Ray C alisema kuathirika kwa dawa za kulevya si janga kwa wasanii pekee, bali hata watu wa kawaida, wakiwemo wafanyakazi serikalini, wafanyabiashara, wapiga debe na wanafunzi.
Msanii huyo alisema mwathirika wa dawa za kulevya ni mgonjwa kama wagonjwa wengine na kwamba mtu anayesema ameathirika maana yake ni kwamba anaumwa.
Alimfananisha mwathirika wa dawa za kulevya kuwa ni sawa na mnywaji wa pombe, ambaye lazima anywe kila siku, asipokunywa anajihisi kama anaumwa. Pia alimfananisha mwathirika wa dawa hizo kuwa ni sawa na mwanaume aliyezoea kulala na mwanamke kila siku, asipofanya hivyo, hajisikii vizuri.
"Watu wengi wanadhani kwamba huyu amejitakia mwenyewe. Huo ni ugonjwa, ukishaingia umeumia, ukitaka kutoka, unashindwa. Kwa hiyo ni ugonjwa kama mwingine na unatibika,"alisema.
"Sikujitakia kuwa mwathirika wa dawa za kulevya, hujui nimeingiaje. Usiseme nimejitakia. Nataka kutoka nashindwa. Naamka asubuhi miguu inauma. Naumwa kama mtu wa kansa. Viungo vyote vinauma. Kwa hiyo nafanyaje? Nipate kidogo ili nipone, lakini si kwamba napenda,"alisema.
Ray C amekiri kuwa, alijitosa katika janga hilo kutokana na kuwa na marafiki wabaya, akiwemo mpenzi wake. Alisema alianza kutumia dawa hizo tangu 2009.
Msanii huyo amewalaani wafanyabiashara wa dawa hizo kwa kuwaelezea kuwa ni watu hatari, lakini mwisho wa siku nao watakufa kama ilivyo kwa 'mateja' wengi.
"Utajenga maghorofa, utakuwa bilionea, lakini hujui siku utakayokufa. Michael Jackson yuko wapi? Si alikuwa milionea?
"Pesa zote utakazokusanya kwa mateja wote wanaoteseka, mwisho wa siku hujui utakufa lini. Utakuwa na pesa, utawatesa watu, lakini laana zote zitakurudia. Pesa zote utaacha, Mungu ndiye atakayewahukumu,"alisema.
Msanii huyo alisema anataka apone kabisa ugonjwa huo ili aweze kutoa somo kwa watanzania wengine kuhusu athari za utumiaji wa dawa za kulevya na pia kurejea upya katika fani ya muziki.
"Nitaingia studio kwa ajili ya mashabiki wangu. Nataka kutoa nyimbo nzuri ili hata kama nikifa, mashabiki wanikumbuke kwa mazuri. Nitafanya shoo nyingi, ninazo nyimbo kama 20 hivi, nimeandika nyimbo nyingi wakati naumwa,"alisema Ray C.
Msanii huyo mahiri katika kukata mauno alisema kimuziki, hakuna msanii anayemtisha na kumsumbua kwa sasa, lakini alikiri kwamba wapo waimbaji wengi wazuri wa kike.
Mwishoni mwa mwaka jana, Ray C alimtembelea Rais Jakaya Kikwete Ikulu ya Dar es Salaam na kumshukuru kwa msaada mkubwa wa matibabu yake, ambayo yanafanyika chini ya uangalizi maalumu.
Ray C alikwenda Ikulu akiwa amefuatana na mama yake mzazi, Margareth Mtweve, ambaye alimshukuru Rais Kikwete kwa msaada huo, ambao alisema umesaidia kurudisha hali ya binti yake.
Rais Kikwete amempongeza Ray C kwa kuikubali hali yake ya kiafya na hatimaye kupata matibabu, ambayo bado anaendelea nayo.
Alimtaka mwanamuziki huyo kufuata masharti ya madaktari ili aweze kupona kabisa na hatimaye kurudia hali yake ya mwanzo na kurejea katika shughuli zake za kujitafutia kipato na maisha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment