'
Saturday, August 24, 2013
YANGA YAUA, SIMBA, AZAM ZACHECHEMEA
YANGA leo imeanza ligi kuu ya Tanzania Bara kwa kishindo baada ya kuibamiza Ashanti mabao 5-1 katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mshambuliaji Jerry Tegete aliibuka shujaa wa Yanga baada ya kuifungia mabao mawili kati ya matano. Mabao mengine yalifungwa na Simon Msuva, Haruna Niyonzima na Nizar Khalfan wakati bao la kujifariji la Ashanti lilifungwa na Shabani Juma.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, Simba ilibanwa mbavu na wenyeji Rhino Rangers baada ya kulazimishwa kutoka nayo sare ya mabao 2-2.
Mabao yote mawili ya Simba yalifungwa na kiungo mchacharikaji, Jonas Mkude wakati mabao ya Rhino Rangers yalifungwa na Iman Niel na Saad Kipanga.
Katika mechi nyingine zilizochezwa leo, Mtibwa Sugar imelazimishwa sare ya 1-1 na Azam FC kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.
Mtibwa ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Juma Luizio dakika ya nne kabla ya Aggrey Morris kuisawazishia Azam kwa penalti dakika ya 19.
JKT Mgambo ilishindwa kutamba kwenye uwanja wake wa nyumbani baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa JKT Ruvu, Coastal Union iliichapa JKT Oljoro mabao 2-0 mjini Arusha, Mbeya City ilitoka suluhu na Kagera Sugar mjini Mbeya, Prisons ilipokea kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Ruvu Shooting
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment