KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 14, 2013

TUTAWAZIBA MDOMO SIMBA-NIYONZIMA



KIUNGO nyota wa klabu ya Yanga, Haruna Niyonzima ametamba kuwa kikosi chake kitawaziba midomo mashabiki wa Simba katika mechi zote mbili za ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu.

Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Niyonzima alisema wamejipanga vyema kuhakikisha kuwa, wanawanyima raha mashabiki wa Simba msimu huu.

Kiungo huyo wa kimataifa wa Rwanda alisema, lengo lao ni kuifunga Simba katika mechi zote mbili za ligi ili waweze kutetea taji lao kwa raha zaidi.

"Unajua mashabiki wa Simba wamekuwa na mazoea ya kutuzomea kila tunapocheza na timu zingine. Sasa ili kuwaziba midomo, lazima tuwafunge mechi zote mbili,"alisema.

Niyonzima alisema tabia hiyo ya mashabiki wa Simba kuwazomea wachezaji wa Yanga, imekuwa ikiwaongezea ari na hamasa ya kufanya vizuri badala ya kuwavunja nguvu.

Hata hivyo, Niyonzima alitabiri kuwa, ligi ya msimu huu itakuwa na ushindani mkali kutokana na usajili mzuri uliofanywa na baadhi ya timu.

Alizitaja timu zinazotarajiwa kutoa upinzani mkali kwa Yanga kuwa ni pamoja na wapinzani wao wa jadi, Simba, Azam, Coastal Union na Mtibwa.

Michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara imepangwa kuanza Agosti 24 mwaka huu. Ligi hiyo itatanguliwa na mechi ya kuwania Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Azam itakayochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment