KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 7, 2013

STEWART AMPIGA DONGO KIM POULSEN


KOCHA Mkuu wa Azam, Stewart Hall amesema kipa namba moja wa timu hiyo, Mwadini Ally ameshuka kiwango kutokana na kuwekwa benchi kwa muda mrefu kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Channel Ten kutoka Afrika Kusini juzi, Stewart alisema tangu alipoteuliwa kuichezea Taifa Stars, Mwadini hajapewa nafasi ya kuichezea katika mechi yoyote ya kimataifa.

Kocha huyo kutoka Uingereza, alitoa kauli hiyo baada ya Azam kuchapwa mabao 3-0 na Kaizer Chief katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa Jumatatu iliyopita mjini Johannesburg.

Stewart alisema licha ya kufungwa, Azam ilicheza vizuri, lakini iliangushwa na Mwadini kutokana na kutokuwa makini katika kulinda lango lake.

"Tumefungwa kutokana na makosa madogo ya kipa na ni kwa sababu hajacheza mechi kwa muda mrefu. Tangu ligi ilipomalizika, amekuwepo kwenye timu ya Taifa, lakini hachezeshwi. Unategemea nini,"alisema kocha huyo.

Kocha huyo ameeleza kufurahishwa kwake na uamuzi wa uongozi wa Azam kuipeleka timu hiyo kambini nchini Afrika Kusini na kuongeza kuwa, ziara hiyo itazidi kuwaimarisha kisoka.

Nahodha wa timu hiyo, Aggrey Morris alisema mipango iliyoandaliwa na uongozi wa Azam katika kuisuka timu hiyo ni mizuri na ni mfano wa kuigwa na klabu zingine za Tanzania.

Morris alisema baada ya kutoka Afrika Kusini, anaamini kuwa kikosi chao kitakuwa kimeimarika kwa ajili ya kushiriki michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, inayotarajiwa kuanza Agosti 24.

No comments:

Post a Comment