KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 7, 2013

COASTAL UNION ITATISHA LIGI KUU-BIN SLUM



UONGOZI wa Coastal Union umetamba kuwa, timu hiyo itatisha katika msimu ujao wa michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara, unaotarajiwa kuanza Agosti 24 mwaka huu.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Coastal, Alhaji Nassor Bin Slum alisema mjini hapa juzi kuwa, wana uhakika huo kutokana na usajili mzuri wa wachezaji walioufanya kwa ajili ya ligi hiyo.

Bin Slum alitoa majigambo hayo baada ya timu hiyo kufanikiwa kumsajili mshambuliaji, Lutimba Yayo kutoka Mamlaka ya Kodi ya Mapato (URA) ya Uganda.

Yayo, ambaye alikuwa mwiba kwa mabeki wa Simba na Yanga wakati URA ilipofanya ziara ya mechi za kirafiki nchini mwezi uliopita, ametia saini mkataba wa kuichezea Coastal kwa miaka miwili.

Kwa mujibu wa Bin Slum, tayari Yayo ameshawasili mjini Tanga na kujiunga na timu hiyo na kuongeza kuwa, walivutiwa na kiwango chake wakati wa ziara ya URA mwezi uliopita.

Katika ziara hiyo, Yayo aliifungia URA mabao mawili ilipoichapa Simba mabao 2-1 kabla ya kuifungia tena timu hiyo mabao mawili ilipotoka sare ya mabao 2-2 na Yanga.

Bin Slum alisema walikamilisha taratibu za kumsajili mchezaji huyo mwanzoni mwa wiki hii baada ya kukutana na viongozi wa URA na mchezaji huyo kwenye hoteli ya Africana iliyopo mjini Kampala.

Alisema usajili huo ulifanywa na mwakilishi wa Coastal Union, Yusuf Akida Saad aliyefunga safari kwenda Uganda kwa ajili ya kazi hiyo.

Hata hivyo, malipo ya ada ya uhamisho wa mchezaji huyo yamefanywa kuwa siri, lakini kuna habari kuwa, URA imeweka kipengele kinachoeleza kuwa, iwapo mchezaji huyo atauzwa kwa klabu nyingine, ipewe asilimia 20 ya pesa za mauzo.

Yayo amekuwa mchezaji wa pili wa URA kuondoka katika klabu hiyo baada ya nahodha, Joseph Owini kujiunga na Simba wiki iliyopita.

Waganda wengine wanaocheza soka ya kulipwa nchini ni Brian Umony wa Azam,
Abel Dhaira wa Simba na Hamisi Kiiza wa Yanga.

No comments:

Post a Comment