KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 7, 2013

MWINYI KAZIMOTO: NAWAOMBA WATANZANIA WANISAMEHE



KIUNGO Mwinyi Kazimoto wa klabu ya Simba na timu ya Taifa, Taifa Stars hivi karibuni alizua gumzo kubwa kwa wadau wa soka nchini baada ya kutoroka kwenye kambi ya timu ya Taifa na kwenda Qatar kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa. Kituo cha redio cha Clouds FM wiki hii kilifanya mahojiano na mchezaji huyo akiwa Qatar kama yalivyonukuliwa na Mwandishi Wetu.


SWALI: Mambo vipi Kazimoto? Unaendeleaje huko?

JIBU: Namshukuru Mungu naendelea vizuri.

SWALI: Je, umefaulu majaribio yako ama bado unaendelea kujaribiwa?

JIBU: Mwanzoni nilipata klabu mbili zinazoshiriki ligi daraja la kwanza ya huku, lakini nikachelewa majaribio na hivyo nikakosa nafasi. Baada ya hapo ndipo ikajitokeza timu ya Al-Markhiya Sports Club - inayoshiriki ligi ya daraja la pili na ikavutiwa na mimi na ikafanya mipango ya kunisajili. Sikuhitajika kufanyiwa majaribio.

SWALI: Kwa hiyo umejiunga na timu hiyo moja kwa moja, inaitwaje?

JIBU: Ndio, inaitwa Al-Marhikiya

SWALI: Unasema ulichelewa kwenda huko, kwani ulitakiwa kufika wakati gani?

JIBU: Safari yangu ya kuja huku Qatar ilibidi iwe kabla hata sijacheza mechi ya marudiano na Ivory Coast, lakini kwa sababu nilikuwa na majukumu, nilivumilia nikabaki mpaka nilipocheza mchezo wa kwanza dhidi ya Uganda, wakati tukiwa kambini kwa ajili ya mchezo wa pili, ikabidi niondoke kwa sababu siku zilikuwa zinaenda na muda wangu wa kufanya majaribio ukawa unaisha. Lakini nikakuta zile timu zimeshapata wachezaji wengine ndio sababu nimelazimika kujiunga na timu ya daraja la pili.

SWALI: Ndio kipindi kile uliondoka timu ya Taifa ikiwa kambini?

JIBU: Ndio.

SWALI: Umetia saini mkataba wa muda gani?

JIBU: Nimetia saini mkataba wa mwaka mmoja. Nisingeweza kusaini mkataba wa muda mrefu kwa sababu timu yenyewe ipo daraja la pili.

SWALI: Ndio kusema umeshamalizana na klabu ya Simba hadi umeamua kuingia mkataba na klabu hiyo?

JIBU: Naona kuanzia leo (Agosti 5) mambo yote yatakuwa sawa.

SWALI: Kuna taarifa kwamba umeamua kutoa sehemu ya pesa zako ulizolipwa kwa ajili ya usajili ili kuvunja mkataba wako na Simba, kwanza nakupongeza kwa tukio la kishujaa kama hilo, je ni kweli?

JIBU: Ni kweli kutokana na kwamba nilikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na Simba, ilibidi nitoe kiasi cha fedha ($40,000 na sio $35,000 kama inavyoripotiwa) kutoka kwenye ada ya usajili wangu kuununua mkataba wangu uliobakia na Simba.
Niliamua kufanya hivyo kwa sababu ya kuangalia maslahi yangu binafsi kwa sababu niliamua kuacha kazi Simba. Naangalia maisha yangu ya baadaye, naangalia mbali zaidi.

SWALI: Umefanya jambo zuri sana Kazimoto,  umelipa dola 40,000 (zaidi ya sh. milioni 45), umezitoa katika sehemu ya fedha zako umeilipa Simba, nadhani ni jambo jema hilo.

JIBU: Sawasawa.

SWALI:Nini mustakabali wako kwa sasa maana tangu ulipoondoka huku, maneno mengi sana yamesemwa na sasa umeshapata timu, nini nafasi yako kwa timu ya Taifa siku zijazo?

JIBU: Kwa vile nimesajiliwa na timu ya daraja la pili, namuomba Mungu aniwezeshe kupata timu ya ligi kuu msimu unaokuja kwa sababu hayo ndiyo malengo yangu makubwa ndio sababu nimesaini mkataba wa mwaka mmoja. Najua nimekuja huku ni mbali, lakini naamini wataniona na nitapata timu ya ligi kuu.

SWALI: Unapenda kuwaeleza nini Watanzania?

JIBU: Niliondoka huko katika kipindi kigumu, nakubali nimekosa, hivyo nawaomba watanzania wote wanisamehe, Simba, TFF na wadau wote wa soka. Nilichokifanya ni kuangalia maisha yangu ya baadaye, sikufanya kitu kibaya sana. Nawaomba watanzania wanisamehe.  

MUHIMU
Habari tulizozpata wakati tukienda mitamboni zimeeleza kuwa, klabu ya Simba imemuuza Kazimoto katika klabu ya Al-Markhiya kwa dau la dola 50,000 (zaidi ya sh. milioni 81).

Mwakilishi wa Al-Markhiya, Saleh Afif alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa,
wametanguliza dola 35,000 (sh. milioni 57) na fedha zilizobaki, dola 15,000 (sh. milioni 24) zitalipwa mwishoni mwa Desemba mwaka huu.

Kwa mujibu wa Afif, mchezaji huyo atakuwa akilipwa mshahara wa dola 7,000 (zaidi ya sh. milioni 11) kwa mwezi kwa kipindi cha mwaka mmoja, atakachokuwa akiichezea timu hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope amethibitisha kuuzwa kwa mchezaji huyo na kuongeza kuwa, hawawezi kumzuia kwa vile anatafuta maisha mazuri zaidi.

Hata hivyo, Hanspope alisema wameionya timu hiyo isirudie kitendo ilichokifanya cha kumtorosha mchezaji huyo kwenye kambi ya Taifa Stars.

No comments:

Post a Comment