KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 14, 2013

WAKALA WA KASEJA ABURUTWA KORTINI



WAKALA wa klabu ya soka ya FC Lumpopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Ismail Banduka, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa tuhuma za kuishi nchini bila kibali.

Banduka, ambaye alikuja nchini kwa ajili ya kushughulikia uhamisho wa kipa Juma Kaseja wa Simba kwenda FC Lupopo, baada ya kusomewa mashitaka yanayomkabili mbele ya Hakimu Mkazi Devotha Kisoka, alikiri makosa hayo.

Awali, akimsomea mashitaka, Wakili Patrick Ngoyomela kutoka Idara ya Uhamiaji, alidai kuwa Agosti 7, mwaka huu, katika eneo la Magomeni Kondoa, Banduka akiwa raia wa Congo, alikutwa akiishi nchini bila ya kibali.

Katika shitaka la pili, Banduka alidaiwa kuwa siku hiyo,  alimdanganya ofisa uhamiaji wa mpaka wa Tunduma kwamba anaingia nchini kwa ajili ya matembezi huku akijua kuwa anaingia kama wakala wa mpira wa miguu.

Banduka pia anadaiwa katika tarehe hiyo, alikutwa akijihusisha na kazi ya uwakala wa mpira wa miguu bila ya kuwa na kibali .

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, Banduka alikiri kutenda makosa hayo na mahakama ilimtia hatiani.

Alipopewa nafasi ya kujieleza kwanini mahakama isimpe adhabu kali, Banduka aliomba apewe adhabu ndogo kwa sababu hakuwa anazijua sheria za uhamiaji za hapa nchini.

Banduka alidai kuwa, aliingia nchini kwa kutumia kibali cha Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), ambacho kinamruhusu kufanya kazi duniani kote.

"Naomba msamaha. Sitarudia kufanya makosa kama hayo tena. Siku nyingine nikija Tanzania, nitaomba kibali hata cha biashara ili niweze kufanya kazi yangu," aliomba Banduka.

Hakimu Hellen alimueleza Banduka kuwa kutojua sheria siyo sababu ya kutenda makosa, ambapo alimpa adhabu ya kifungo cha miezi mitatu jela kwa kila kosa au kulipa faini ya sh.150,000.
Banduka alilipa faini hiyo na kuachiwa huru, hivyo kunusurika kifungo cha miezi tisa jela.

No comments:

Post a Comment