KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, August 5, 2013

KASEJA: BADO SIJAMWAGA WINO FC LUPOPO, NASUBIRI KUONA MKATABA



KIPA wa zamani wa klabu ya Simba, Juma Kaseja amesema bado hajamalizana na klabu ya FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuhusu usajili wake msimu ujao.



Kaseja amesema mjini Dar es Salaam leo kuwa, ameshafanya mazungumzo ya awali na uongozi wa FC Lupopo na kukubaliana kuhusu malipo ya mshahara, lakini hajatia saini mkataba wa kuichezea klabu hiyo.



"Kimsingi nimezungumza nao (viongozi wa FC Lupopo) na kukubaliana kuhusu malipo ya mishahara na marupurupu mengine, lakini sijatia saini mkataba kwa sababu siwezi kufanya hivyo bila ya kuuona,"alisema.

Kwa mujibu wa Kaseja, anatarajia kuondoka nchini mwishoni mwa wiki hii kwenda DRC kwa ajili ya kuusoma mkataba alioandaliwa na uongozi wa klabu hiyo kabla ya kutia saini.

Kwa upande wake, Meneja wa FC Lupopo, Balanga Ismail amesema anashukuru kwamba mazungumzo kati yao na Kaseja yamekwenda vizuri na kusisitiza kuwa, atakuwa kipa namba moja wa klabu hiyo.

Ismail alisema kwa sasa FC Lupopo haina kipa wa uhakika na kuongeza kuwa, kusajiliwa kwa Kaseja huenda kukamaliza tatizo hilo.

Alimwelezea Kaseja kuwa ni kipa mahiri katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati na anajulikana na kusifika kutokana na uwezo wake wa kulinda lango.

Kuna habari kuwa, FC Lupopo imeahidi kumpa Kaseja kitita cha dola 30,000 za Marekani (zaidi ya sh. milioni 30) kwa ajili ya kuichezea timu hiyo msimu ujao.

Mkataba wa Kaseja kuichezea Simba ulimalizika mwishoni mwa msimu uliopita na uongozi wa klabu hiyo ulikataa kumuongezea mkataba mwingine.

Mbali na Kaseja, wachezaji wengine walioachwa na klabu hiyo ni Haruna Moshi na Juma Nyoso waliojiunga na Coastal Union ya Tanga.

No comments:

Post a Comment