KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 29, 2013

YANGA YABANWA, MABOMU YARINDIMA


MABINGWA watetezi Yanga jana walilazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Coastal Union katika mechi ya ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga itabidi ijilaumu kwa kushindwa kutoka uwanjani na ushindi kwani ilikuwa ikiongoza kwa bao 1-0 hadi dakika ya 87 wakati Coastal Union ilipopata adhabu ya penalti na kusawazisha.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbagu aliifungia Yanga bao la kuongoza dakika ya 67 kwa shuti kali baada ya kupokea pasi kutoka kwa beki David Luhende.

Coastal ilisawazisha kwa njia ya penalti kwa bao lililofungwa na Jerry Santo baada ya kutokea madhambi kwenye lango la Yanga.

Katika mchezo huo, mwamuzi Martine Saanya wa Pwani aliwatoa nje kwa kadi nyekundu Simon Msuva wa Yanga na Crispine Odula dakika ya 73 kwa mchezo mbaya.

Licha ya timu zote mbili kuchuana vikali dakika 45 za kipindi cha kwanza, hakuna iliyoweza kupata bao. Kila timu ilipata nafasi nzuri za kufunga, lakini umaliziaji mbovu ulikuwa kikwazo.

Coastal ilianza mchezo kwa kasi dakika ya kwanza baada ya Uhuru Selemani, kuchomoka na mpira na kupiga krosi iliyoshindwa kuunganishwa na Christipine Odula aliyepiga shuti nje.

Yanga ilijibu shambulizi hilo dakika ya nane lakini Msuva alishindwa kufunga baada ya kupiga mpira wa kichwa dhaifu licha ya kupata pasi nzuri ya kiungo, Salum Telela.

Haruna Moshi 'Boban' alishindwa kuipa Coastal Union bao dakika ya 67 baada ya kuzembea na mpira akiwa ndani ya eneo la hatari kabla ya mabeki wa Yanga kuokoa hatari.

Dakika ya 69 Deo Lyanga wa Coastal Union alishindwa kufunga baada ya kupiga shuti juu.
Mbali na kutoa kadi nyekundu, Saanya aliwaonya kwa kadi za njano wachezaji Kavumbagu wa Yanga na beki Juma Saidi 'Nyoso' wa Coastal kwa mchezo wa rafu.

Baada ya pambano hilo kumalizika, mashabiki wa Yanga walizingira eneo la mlango wa kuingilia uwanjani wakitaka kumpiga mwamuzi Saanya. Pia walirusha mawe kwenye basi lililowabeba wachezaji wa Coastal Union na kusababisha mchezaji mmoja ajeruhiwe kichwa.

Polisi walilazimika kufyatua mabomu ya machozi kuwatawanya mashabiki hao.

Yanga: Ali Mustapha, Juma Abdul, David Luhende, Nadir Haroub, Mbuyu Twite, Salum Telela/Hamis Thabit, Simon Msuva, Frank Domayo, Didier  Kavumbagu, Jerry Tegete/Hussein Javu, Haruna Niyonzima.

Coastal:  Shaaban Kado,  Juma Hamad, Abdi Banda, Marcus  Ndeheli, Juma Nyoso, Jerry Santo, Uhuru Selemani/ Selemani Kassim, Christipine Odula, Yayo Tutimba, Haruna Moshi na Danny Lyanga.

No comments:

Post a Comment