'
Thursday, October 24, 2013
RONALDO DE LIMA: HAKUNA ANAYEWEZA KUFUTA REKODI YANGU
ZURICH, Uswisi
MEI 25, 1993, Ronaldo Luis Nazario de Lima alianza kuandika ukurasa mpya katika maisha yake kisoka. Akiwa na umri wa miaka 16, aliichezea timu ya Cruzeiro dhidi ya Caldense katika michuano ya kuwania ubingwa wa Jimbo la Minas Gerais nchini Brazil, akiwa na wanasoka kadhaa maarufu wa kulipwa.
Kutokana na umahiri wake wa kusakata kabumbu, Ronaldo alipachikwa majina mengi ya utani kama vile 'O Fenomeno' na ni mmoja wa wachezaji wa aina yake kutokea duniani.
Hadi sasa, Ronaldo anashikilia rekodi ya kufunga mabao 15 katika fainali za Kombe la Dunia na amewahi kuzichezea klabu kadhaa maarufu duniani kama vile PSV Eindhoven ya Uholanzi, Barcelona ya Hispania, Inter Milan na AC Milan za Italia na Real Madrid ya Hispania.
Mwaka huu, Ronaldo ametimiza miaka 20 tangu alipoanza kucheza soka ya kulipwa. Anaikumbuka vyema siku alipopewa nafasi kwa mara ya kwanza ya kuichezea Cruzeiro, akiwa kinda mwenye umri wa miaka 16.
"Ni muda mrefu uliopita. Nakumbuka kila kitu kuhusu maisha yangu kisoka, kuanzia tangu mwanzo, kama vile ilikuwa jana. Nakumbuka jinsi nilivyojisikia nilipoanza kuicheza soka ya kulipwa Cruzeiro. Siku zote nilikuwa na ndoto ya kuwa mwanasoka na ilifurahisha nilipogundua ndoto hiyo ilianza kuwa kweli. Ilikuwa kama vile uchawi. Miguu, mikono na viganja vyangu vilikuwa vikitetemeka. Lakini baada ya mchezo kuanza, nilitulia,"alisema Ronaldo.
Mwanasoka huyo anasema, baada ya kuelezwa na kocha kwamba angecheza mechi hiyo, alichanganyikiwa na moyo wake ulianza kwenda mbio, lakini hicho ndicho alichokuwa akikitaka.
"Niliweza kutulia na kuwa katika hali ya kawaida. Kwa kawaida, wachezaji hupatwa na kimuhemuhe kabla ya mchezo, lakini baadaye kinatoweka. Unasahau kila kitu unapokuwa kwenye mchezo,"alisema.
Kutokana na kutokuwepo kwa simu za mkononi wakati huo, Ronaldo hakuweza kuwapa taarifa rafiki zake waliokuwa wakiishi Bento Ribeiro, jirani na Rio de Janeiro. Pia hawakuwa na simu za kawaida katika nyumba walizokuwa wakiishi.
Aliwapa taarifa hizo wazazi na ndugu zake, nao wakazisambaza kwa rafiki zake na watu wengine. Kila mmoja alikuwa na hamu kubwa ya kumshuhudia kwa macho akisakata kabumbu katika moja ya klabu kubwa na maarufu nchini Brazil.
Kwa mujibu wa Ronaldo, mechi hiyo haikuonyeshwa kwenye televisheni. Baba yake alilazimika kwenda sehemu fulani ya mji aliokuwa akiishi na kupanda juu ya mlima, ambako aliwasha redio yake na kusikiliza mechi hiyo moja kwa moja. Cruzeiro ilishinda mechi hiyo.
Ronaldo anakumbuka vyema kwamba, mshahara wake wote wa kwanza alimpatia mama yake mzazi kwa vile ndiye aliyempatia sofa kwa ajili ya kulalia walipokuwa wakiishi Bento Ribeiro.
Mwanasoka huyo nyota wa zamani anasema, kutokana na nidhamu aliyokuwa nayo wakati akicheza soka, hakuweza kufanya vitendo, ambavyo vingeharibu maisha yake ama kuchafua jina lake.
"Kila kitu kilikwenda vizuri kama nilivyotaka. Kiukweli, mambo yalikuwa mazuri kuliko nilivyotarajia. Kamwe sikufikiria iwapo ningefika mbali. Siku zote nilikuwa na ndoto ya kuwa mwanasoka tu,"alisema Ronaldo.
Nyota huyo wa zamani wa Brazil anasema, hali ilianza kuwa ngumu kwake baada ya kuondoka Brazil akiwa na umri wa miaka 17 na kwenda Uholanzi kwa vile maisha yalikuwa tofauti. Tatizo kubwa aliloanza kukumbana nalo ni mabadiliko ya hali ya hewa.
Ronaldo anasema kila kitu mwilini mwake kilikuwa kama vile kimeganda, kuanzia miguu, mikono, shingo na masikio. Hali hiyo ilikuwa ikimtokea zaidi alipokuwa mazoezini. Kamwe hakuwaza kuishi katika nchi yenye baridi kali.
Tatizo lingine lilikuwa kwenye chakula na lugha. Hakuweza kuzungumza Kidachi. Ilikuwa vigumu kwake kuchagua aina ya chakula alichotaka kula kwenye 'menyu'. Ilikuwa vigumu kwake kujifunza lugha hiyo.
"Ilinichukua miaka miwili kujifunza lugha na kuielewa na sasa nimeshaisahau kwa vile sijaizungumza kwa muda mrefu. Lakini nilifurahia kuwepo uwanjani,"alisema Ronaldo.
Nyota huyo wa Brazil amewataja wanasoka waliokuwa wakimvutia kuwa ni pamoja na Zico na Marco van Basten wa Uholanzi. Anasema wanasoka hao wawili walikuwa miongoni mwa washambuliaji bora duniani.
Ronaldo anasema maamuzi yote aliyowahi kuyafanya wakati akicheza soka ya kulipwa yalikuwa mazuri na yaliweza kubadili maisha yake. Ameyataja maamuzi hayo kuwa ni kujiunga kwake na klabu za Cruzeiro, PSV Eindhoven, Barcelona, Inter Milan na zinginezo alizowahi kuzichezea.
Mwanasoka huyo anasema, hakuna timu aliyokuwa akipenda kuichezea, akashindwa kufanya hivyo. Anasema alitamani kwenda kucheza soka England, lakini haikuwezekana.
Licha ya kuchezea klabu kubwa kama vile Barcelona na Real Madrid, Ronaldo anasema hajali iwapo baadhi ya watu hawakufurahishwa na kiwango chake. Anasema anachotambua ni kwamba, mashabiki wengi walifurahishwa na staili yake ya uchezaji.
Ronaldo alikuwemo kwenye kikosi cha Brazil kilichotwaa Kombe la Dunia nchini Marekani, lakini hakucheza mechi hata moja. Aliitwa kwenye kikosi hicho kwa ajili ya kupata uzoefu kwa vile kilikuwa kikiundwa na washambuliaji wengi nyota kama vile Romario, Bebeto, Dunga, Rai na Leonardo.
Anasema alikuwa akifurahia kuwaona wachezaji hao kwenye TV, lakini baada ya kuwa nao kwenye kikosi kimoja, furaha yake iliongezeka. Anasema alipata nafasi nzuri ya kujifunza mengi kutoka kwao na pia kucheza nao pamoja.
"Nakumbuka wakati wa mazoezi, nilikuwa nikiwatazama Romario na Bebeto wanavyocheza. Ilikuwa sehemu nzuri ya kujifunza kucheza soka,"alisema.
Akizungumzia fainali zijazo za Kombe la Dunia, zitakazofanyika 2014 nchini Brazil, Ronaldo anasema kikosi cha sasa cha timu hiyo ni tofauti na vya miaka iliyopita. Lakini anakiri kwamba, kikosi hicho kimeonyesha mabadiliko makubwa wakati wa michuano ya Kombe la Mabara.
Ronaldo anasema ushindi wa Brazil katika michuano ya Kombe la Mabara, umewapa faraja kubwa mashabiki kwamba, huenda wakafanikiwa kutwaa Kombe la Dunia nyumbani.
"Tunayo nafasi kubwa,"alisisitiza nyota huyo, ambaye anamiliki vitega uchumi kadhaa, ikiwa ni pamoja na kununua hisa kwenye kampuni mbalimbali.
Ronaldo ametoa nafasi kubwa kwa timu za Hispania na Ujerumani kutwaa kombe hilo mwakani. Lakini pia ametoa nafasi hiyo kwa timu yake ya Brazil kwa vile itakuwa ikicheza nyumbani.
"Naweza kusema kwamba, timu zenye nafasi kubwa ni Brazil, Ujerumani na Hispania,"amesema nyota huyo.
Ronaldo anatambua vyema kwamba, mshambuliaji Miroslav Klose wa Ujerumani anaweza kufikia rekodi yake iwapo atafunga bao katika fainali hizo. Klose ameweka rekodi ya kufunga mabao 14 katika fainali za kombe hilo.
"Sina wasiwasi wa kuvunjwa kwa rekodi yangu. Siku zote naamini kwamba, rekodi zinaweza kuvunjwa. Ipo siku atatokea mtu wa kuvunja rekodi hiyo,"alisema Ronaldo.
"Nilitengeneza jina langu kwa sababu ya kufunga magoli na hilo haliwezi kusahaulika. Historia yangu binafsi na mabao 15 niliyofunga katika Kombe la Dunia, kamwe haviwezi kufutika,"alisisitiza.
"Kama atafunga mabao zaidi yangu, nitampongeza na ni mwanasoka ninayevutiwa naye. Lakini kamwe hawezi kufuta historia yangu na mabao yangu," aliongeza.
Iwapo Klose atafanikiwa kuifikia ama kuvunja rekodi hiyo, itakuwa ni sawa na kulipiza kisasi kwa Wajerumani baada ya Ronaldo kuvunja rekodi ya Gerd Muller.
"Inawezekana rekodi ikarejea Ujerumani. Lakini ni rekodi inayoleta mafanikio binafsi, sio ushindi wa timu. Rekodi inaisaidia timu, lakini kitu muhimu ni kupata ushindi wa pamoja,"alisema Ronaldo.
Ronaldo amewataka wanasoka wanaochipukia kuwa na subira, malengo na nidhamu. Anasema binafsi hajabadilika kitu kwa vile bado anafanya mambo yale yale aliyokuwa akiyafanya wakati akicheza soka ya kulipwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment