'
Thursday, October 10, 2013
KIBADENI, JULIO WAKALIA KUTI KAVU SIMBA
WAKATI homa ya pambano la watani wa jadi wa soka nchini, Simba na Yanga ikiwa imeshaanza kupanda, hali si shwari kwa klabu ya Msimbazi baada ya wachezaji kuanza kulitupia lawama benchi lao la ufundi.
Uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, baadhi ya wachezaji wa timu hiyo wameanza kuchoshwa na vitendi vya Kocha Mkuu, Abdalla Kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo 'Julio'na kutaka waondolewe.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, makocha hao wamekuwa wakiwafokea hovyo wachezaji wanapokuwa kambini na uwanjani na hivyo kuwakosesha raha.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao, baadhi ya wachezaji walisema, uongozi umekuwa ukiwapa ahadi nyingi za malipo yao, lakini umeshindwa kuzitekeleza.
"Hali hii imechangia kushusha ari yetu na kucheza kwa kujituma kwa sababu hatuna uhakika na malipo yetu,"alisema mmoja wa wachezaji hao.
Aliongeza kuwa, tangu kuanza kwa ligi hiyo, wamekuwa wakilipwa pesa kiduchu, tofauti na makubaliano kati yao na uongozi, ambapo timu ikishinda, wanalipwa asilimia 50 ya mapato, ikitoka sare wanalipwa asilimia 40 na ikifungwa hawapati kitu.
Kwa mujibu wa wachezaji hao, kuna wakati mmoja wa viongozi wa juu wa klabu hiyo amekuwa akiwapelekea malipo yao uwanjani kabla ya kuanza kwa mechi za ligi.
Akitoa mfano, mmoja wa wachezaji hao alisema, kiongozi huyo aliwapelekea pesa zao uwanjani kabla ya Simba kucheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.
"Alikuja uwanjani, akamkabidhi pesa Amri Kiemba, naye akampelekea Nico Nyagawa, ambaye alizigawa kwa wachezaji,"alisema mchezaji huyo.
Habari zingine zimeeleza kuwa, wachezaji wa timu hiyo walilazimika kwenda kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kusubiri mgawo wao baada ya mechi kati yao na Ruvu Shooting, ambapo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
"Kingine kinachotukera na kutuvunja nguvu ni kwamba, tumekuwa tukifokewa kama watoto wadogo kila tunapofanya makosa uwanjani au wakati wa mazoezi. Hali hii inatuvunja nguvu sana,"alisema mchezaji mwingine wa timu hiyo.
Pamoja na kuwepo kwa malalamiko hayo kutoka kwa wachezaji, Kibadeni na Julio wameiwezesha Simba kuongoza ligi hadi sasa, ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi saba, ikifuatiwa na Yanga na JKT Ruvu zenye pointi 12 kila moja.
Kibadeni aliteuliwa kuwa kocha wa Simba, baada ya kuiwezesha Kagera Sugar kushika nafasi ya nne msimu uliopita. Kibadeni amechukua nafasi ya kocha wa zamani, Patrick Liewig kutoka Ufaransa.
Juhudi za kumtafuta Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage ili azungumzie shutuma hizo, hazikuweza kuzaa matunda kutokana na simu yake ya mkononi kuita kwa muda mrefu bila kupokelewa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment