KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 10, 2013

SIMBA, YANGA HAZITABIRIKI-MAKOCHA


Juma Mwambusi-Mbeya City
Charles Boniface-Ruvu Shooting

BAADHI ya makocha wa timu zinazoshiriki michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara, wamesema ni vigumu kutabiri timu ipi kati ya Simba na Yanga, itakayoshinda pambano lao litakalochezwa Oktoba 20 mwaka huu.

Wakizungumza na Burudani kwa nyakati tofauti mjini Dar es Salaam jana, makocha hao walisema viwango vya timu hizo kwa sasa vipo juu na pambano kati yao litakuwa na ushindani mkali.

Hata hivyo, makocha hao walikiri kuwa, kikosi cha Simba kinaundwa na wachezaji wengi wapya na wenye umri mdogo, tofauti na Yanga yenye wachezaji wengi wazoefu wa ligi na michuano ya kimataifa.

Kocha Mkuu wa JKT Ruvu, Mbwana Makata amekisifu kikosi cha Simba kwa kusema kuwa, kutokana na kuundwa na vijana wengi wadogo, wanacheza kwa kasi muda wote wa mchezo.

Makata alisema anaamini iwapo Kocha Mkuu wa Simba, Abdalla Kibaneni atapewa muda zaidi wa kukinoa kikosi hicho, kitakuwa tishio katika ligi.

"Simba ni wazuri sana, nimecheza nao na kugundua kwamba wana kikosi imara.
Yanga nao sio wabaya, lakini nimeona kama bado kidogo wana kasoro kwenye sehemu ya ushambuliaji, wanapoteza nafasi nyingi za kufunga mabao na wakati mwingine ngome yao inakatika wakati wakishambuliwa na kuruhusu mabao ya kizembe,"alisema Makata.

Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa, amekiri kwamba timu hizo zinaundwa na wachezaji wengi wazuri, lakini hakuwa tayari kubashiri matokeo ya mechi kati yao.

Hata hivyo, Mkwasa amesema timu hizo bado zina matatizo makubwa kwenye safu zake za ushambuliaji kutokana na washambuliaji wake kutokuwa makini katika kufunga mabao.

Mkwasa alisema pambano kati ya watani hao wa jadi litakuwa na ushindani mkali na timu yoyote inaweza kushinda. Alisema mara nyingi matokeo ya mechi kati ya Simba na Yanga hayategemei ubora wa timu.

Kocha Mkuu wa Mbeya City, Juma Mwambusi amesema timu hizo zinaundwa na wachezaji wengi wazuri, na kuongeza kuwa, yoyote inaweza kushinda pambano la Oktoba 20.

Hata hivyo, Mwambusi anapinga sera za timu hizo kusajili wachezaji kutoka nje kwa madai kuwa, zimepitwa na wakati. Amesema Tanzania inayo hazina kubwa ya wachezaji wenye vipaji vya kucheza soka.

No comments:

Post a Comment