Kikosi cha Yanga
Kikosi cha Simba
WACHEZAJI Betram Mwombeki, Joseph Owino na Gilbert Kaze jana walirejesha
heshima ya Simba baada ya kuifungia mabao ya kusawazisha katika mechi ya ligi
kuu ya Tanzania Bara dhidi ya watani wao wa jadi Yanga.
Katika mechi hiyo, iliyokuwa na ushindani mkali na msisimko wa aina yake,
iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, timu hizo kwenye nchini na
zenye utani wa jadi, zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya mabao 3-3.
Yanga itabidi ijilaumu kwa kushindwa kutoka uwanjani na ushindi baada ya kuwa
mbele kwa mabao 3-0 hadi mapumziko.
Bao la kwanza la Yanga lilifungwa na Mrisho Ngasa dakika ya 12 kwa mpira wa
kuparaza baada ya kupokea pasi kutoka kwa Didier Kavumbagu.
Hamisi Kiiza aliiongezea Yanga bao la pili dakika ya 36 baada ya mabeki wa Simba
kuzembea kuokoa mpira uliopigwa kwenye lango lao.
Dakika moja kabla ya mapumziko, Kiiza aliiongezea Yanga bao la tatu baada ya
gonga nzuri kati ya Kavumbagu na Ngasa.
Mmoja wa mashabiki waliozimia uwanjani akibebwa kwenye machela
Kipindi cha pili kilipoanza, wachezaji wa Yanga walionekana kuridhika na ushindi wa
mabao 3-0 walioupata na hivyo kucheza kwa kurilaksi.
Kuona hivyo, Kocha Abdalla Kibadeni aliamua kuwatoa Abdulrahim Humud na
Haruna Chanongo na kuwaingiza Saidi Ndemla na William Lucian, ambao waliongeza
uhai kwenye safu ya kiungo.
Mwombeki aliifungia Simba bao la kwanza dakika ya 53 baada ya kuwatoka mabeki
wa Yanga na kufumua kiki kali iliyotinga wavuni.
Owino aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 56, kufuatia mpira wa adhabu uliopigwa
na Ramadhani Singano kabla ya Kaze kufunga la tatu dakika ya 75.
Simba: Abel Dhaira, Nassoro Masoud 'Cholo', Haruna Shamte, Gilbert Kaze, Joseph
Owino, Jonas Mkude, Ramadhani Singano, Abdulrahim Humud/William Lucian,
Betram Mwombeki, Amisi Tambwe, Haruna Chanongo/Saidi Ndemla.
Yanga: Ali Mustafa 'Barthez', Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub
'Cannavaro', Kelvin Yondan, Athumani Iddi 'Chuji', Haruna Niyonzima, Frank
Domayo, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngasa, Hamisi Kiiza.
Wakati huo huo, mashabiki wapatao 20 jana walizimia uwanjani wakati Simba na
Yanga zilipokuwa zikimenyana.
Mashabiki hao walianza kuzimia baada ya Yanga kufunga bao la pili na wengine
baada ya Simba kufunga bao la pili na hatimaye kusawazisha.
Furaha ya ushindi. Wachezaji wa Yanga wakifurahia baada ya kupata bao la tatu
Shabiki huyu mwanamke akiwa amezimia
No comments:
Post a Comment