KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 10, 2013

MATAJIRI WATANO KUIBEBA YANGA


Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Yussuf Manji akiteta jambo na mmoja wa wajumbe wa sekretarieti ya klabu hiyo, Patrick Naggi.

MATAJIRI watano wa klabu ya Yanga wamekabidhiwa jukumu la kuisimamia timu hiyo na kuhakikisha inashinda mechi zote zilizosalia za michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara na kutwaa ubingwa.
Jukumu la matajiri hao linaanzia katika mechi dhidi ya Kagera Sugar, itakayochezwa keshokutwa mjini Bukoba na kufuatiwa na mechi dhidi ya Simba, itakayochezwa Oktoba 20 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matajiri waliopewa jukumu hilo ni Abdalla Bin Kleb, Davis Mosha, Ahmed Seif 'Magari', Mussa Katabalo na mfanyabiashara mmoja kutoka Rwanda, ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, matajiri hao walikuwa na kikao kizito kilichofanyika juzi usiku kwenye hoteli moja kubwa mjini Dar es Salaam. Kikao hicho kilifanyika kwa saa nne, kuanzia saa mbili hadi saa sita usiku.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa, matajiri hao wataunda kamati ya ushindi ya Yanga, itakayokuwa chini ya Bin Kleb, ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya usajili, inayoongozwa na Seif.
Katika kikao hicho, iliamuliwa kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji akae pembeni na kushughulikia masuala mengine muhimu, yakiwemo kusimamia ujenzi wa uwanja wa kisasa wa soka eneo la Jangwani, Dar es Salaam.
"Kimsingi tumekubaliana kwamba, Yanga sasa itakuwa chini ya kamati hii hadi ligi itakapomalizika. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa tunashinda mechi zote na kutwaa ubingwa," alisema mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
"Tumechoka kuona timu ikifungwa ama kutoka sare. Pia tunataka kuvunja mwiko wa kufungwa ama kuambulia sare kwa Kagera Sugar kule Bukoba. Tunataka kuona safari hii tunaondoka Bukoba na pointi zote tatu," alisema mjumbe huyo.
Miongoni mwa mikakati iliyowekwa na kamati hiyo ni kutoa zawadi nono kwa wachezaji kila watakaposhinda mechi za ligi. Zawadi hizo ni pamoja na kitita cha sh. milioni moja kwa kila mchezaji atakayefunga ama kusababisha bao.
Mjumbe huyo, ambaye ni kipenzi kikubwa cha wachezaji alisema, wajumbe wa kamati hiyo wanatarajiwa kuongozana na timu kwenda Bukoba leo. Timu hiyo imepanga kwenda Bukoba kwa ndege leo alfajiri.
"Tunataka kuvunja makundi yote ndani ya Yanga na kuona wachezaji wanahamasika kuitumikia timu yao. Na kamati hii haitavunjwa, itaendelea na majukumu yake hadi ligi itakapomalizika,"alisema mjumbe huyo.
Pambano kati ya Yanga na Kagera Sugar linatarajiwa kuwa na upinzani mkali kutokana na kila moja kupania kushinda ili kuchupa nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Katika mechi ya kwanza ya ligi hiyo msimu uliopita, Yanga ilipigwa mweleka wa bao 1-0 na Kagera Sugar mjini Bukoba kabla ya kushinda idadi hiyo ya bao katika mechi ya marudiano iliyochezwa mjini mjini Dar es Salaam.
Kwa sasa, Yanga inashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 12 baada ya kucheza mechi saba, sawa na JKT Ruvu, inayoshika nafasi ya tatu. Simba inaongoza kwa kuwa na pointi 15.

No comments:

Post a Comment