KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, October 6, 2013

SIMBA CHUPUCHUPU KWA RUVU SHOOTING, PAMBANO LAINGIZA MIL 75/-



SIMBA jana iliponea chupuchupu kuadhiriwa na Ruvu Shooting baada ya kulazimishwa kutoka nayo sare ya bao 1-1 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ruvu Shooting ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 15 lililofungwa na Saidi Dilunga baada ya kuwazidi mbio mabeki Joseph Owino na Gilbert Kaze wa Simba. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

Mrundi, Hamisi Tambwe aliisawazishia Simba kwa njia ya penalty dakika ya 52 baada ya Betram Mombeki kuangushwa ndani ya eneo la hatari.

Kwa matokeo hayo, Simba bado inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi saba, ikifuatiwa na JKT Ruvu yenye pointi 12, Azam, Coastal Union, Mbeya City na Kagera Sugar zenye pointi 11 kila moja.

Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Coastal Union ilitoka suluhu na Azam, Mbeya City iliichapa JKT Oljoro mabao 2-1 wakati JKT Ruvu iliichapa Kagera Sugar 2-0.


PAMBANO LA RUVU, SIMBA LAINGIZA MIL 75/-
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya wenyeji Ruvu Shooting na Simba lililochezwa jana (Oktoba 5 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 75,692,000.

Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo namba 43 la VPL msimu wa 2013/2014 lililomalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 walikuwa 13,395.

Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 17,983,902.31 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 11,546,237.29.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 9,144,357.11, tiketi sh. 3,183,382, gharama za mechi sh. 5,486,614.26, Kamati ya Ligi sh. 5,486,614.26, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,743,307.13, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) sh. 1,066,841.66 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,066,841.66.
 
UAMUZI KAMATI YA MAADILI KUFANYIWA MAPITIO
Shirikisho liko kwenye hatua za mwisho za mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 26/27 Oktoba 2013 hapa jijini Dar es salaam.
 
Hivi sasa, wagombea wanasubiri vyombo vya juu vya uamuzi kwa ajili ya kutoa uamuzi wa mwisho kabla ya kuanza kampeni na hatimaye uchaguzi.
 
Hata hivyo, baada ya Kamati ya Maadili kufanya uamuzi dhidi ya kesi nane zilizowasilishwa mbele yake, Sekretarieti imeona kuwepo kwa ukakasi katika utekelezaji wa uamuzi huo kutokana na ukweli kuwa kuna baadhi ya mambo yanaonekana kuwa na ugumu katika kuyatekeleza.
 
Sekretarieti si chombo chenya mamlaka ya kutafsiri uamuzi wa vyombo huru vya Shirikisho, kazi yake kubwa ni kupokea uamuzi na kuutekeleza, hivyo kwa kuwa kuna ukakasi huo imeamua kuwasilisha uamuzi huo kwenye Kamati ya Rufani ya Maadili kwa ajili ya kuufanyia mapitio (revision) na pia kutoa mwongozo kabla ya kurejesha uamuzi huo kwenye Kamati ya Uchaguzi kwa ajili ya kuendelea na mchakato.
 
Sekretarieti imefanya hivyo kwa lengo la kusaidia wagombea ambao wengi wanaonekana kuwa njia panda baada ya kupokea uamuzi wa Kamati ya Maadili na kuiuliza Sekretarieti kuwa inakuwaje Kamati ya Maadili iwaone hawana hatia, lakini hapo hapo ikubaliane na uamuzi wa kuwaengua, jambo ambalo kwa kweli limetufanya tukose majibu sahihi na hivyo kuamua kuomba revision na mwongozo.
 
Pia mwongozo utakaotolewa na Kamati ya Rufani ya Maadili utasaidia kuweka mwelekeo mzuri wa masuala ya Maadili katika siku zijazo.
 
Miongoni mwa mambo yanayoonekana kuwa na ukakasi ni kuwaona watu wote ambao kesi zao ziliwasilishwa kwenye Kamati ya Maadili hawana hatia, lakini hapo hapo kukubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi wa kuwaengua baadhi yao kwa sababu za kinidhamu ikisema haiwezi kuwahukumu mara mbili kwa kuwa wameshaadhibiwa kwa kuenguliwa kwenye uchaguzi.
 
Ili haki itendeke na ionekane inatendeka, Sekretarieti imeona ni vizuri masuala hayo yakafanyiwa revision (mapitio) na kutolewa mwongozo ili kuondoa ukakasi uliojitokeza miongoni mwa wagombea, Shirikisho na wadau na hivyo kujenga hisia kuwa kuna mbinu zimefanyika dhidi ya baadhi ya wagombea.
 
Uamuzi huu haumaaniishi kuwa Sekretarieti inapingana na uamuzi wa Kamati ya Maadili, bali ni utaratibu wa Sekretarieti kuomba ufafanuzi au mwongozo kutoka vyombo husika pindi inapotokea ukakasi katika utekelezaji wa uamuzi wa vyombo vya uamuzi vya Shirikisho.
 
Sekretarieti imeshamwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani za Maadili ili aitishe kikao kwa manajiri ya kufanya mapitio na kutoa mwongozo ambao utasaidia Shirikisho kuendelea na uchaguzi bila ya ukakasi.
 
SERIKALI, TAASISI ZAOMBWA KUISAIDIA U20 WANAWAKE
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeiomba Serikali, taasisi na kampuni mbalimbali kuisaidia timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 inayojiwinda kwa mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya Msumbiji.
 
Timu hiyo hivi sasa iko kambini Mlandizi mkoani Pwani chini ya Kocha Rogasian Kaijage kujiandaa kwa mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza itakayochezwa Oktoba 26 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Miguu ya Wanawake ya TFF, Lina Kessy amesema hiki ndio kipindi muafaka cha kuisaidia timu hiyo ili iweze kufanya vizuri katika mashindano hayo.
 
Ameitaka jamii kujitokeza kuisaidia timu hiyo ambayo haina mdhamini wala mfadhili, kwani timu za Taifa ni za Watanzania badala ya kusubiri ifanye vibaya na kusema ni kichwa cha mwendawazimu.
 
Kessy ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA), ameishukuru kambi ya JKT Ruvu kwa kutoa fursa ya kambi kwani timu hiyo hailipii malazi badala yake inalipia huduma nyingine inazopata hapo.
 
Vilevile amewashukuru wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakijitolea kutokana na ukweli kuwa tangu kuanza mashindano ya mpira wa miguu wa wanawake kumekuwepo uungwaji mkono mkubwa.
 
“Shukrani za kipekee kwa wazazi kukubali watoto wao wachezee timu ya Taifa, kwani wengi bado wanasoma na wapo chini ya uangalizi wa wazazi. Pia tunawaomba wazazi wajitokeze mazoezini ili kuwajenga kisaikolojia wachezaji wetu,” amesema.
 
Fainali za Dunia za U 20 kwa wanawake zitafanyika mwakani nchini Canada. Iwapo Tanzania itaitoa Msumbiji katika raundi hiyo, raundi inayofuata itacheza na mshindi kati ya Botswana na Zimbabwe.
 
WASHABIKI WENYE SILAHA MARUFUKU VIWANJANI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia Jeshi la Polisi kuanzia sasa halitashikilia silaha za washabiki, na badala yake litawazuia kabisa kuingia viwanjani wakati wa mechi.
 
Jeshi la Polisi limekuwa likihifadhi silaha za washabiki wanaokwenda viwanjani, na baadaye kuwarejeshea baada ya mechi kumalizika kwa vile Kanuni za Usalama Viwanjani za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) zinakataza silaha viwanjani.
 
Wikiendi iliyopita katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jeshi la Polisi lilikamata bastola 17 katika upekuzi wa washabiki waliokwenda kushuhudia mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting na ile kati ya JKT Ruvu na Simba. Wote waliokutwa na silaha hizo walikuwa na leseni za kuzimiliki.
 
Hivyo, kwa washabiki wanaomiliki silaha hatawaruhusiwa kabisa kuingia viwanjani, na badala yake tunawashauri kuzihifadhi huko wanakotoka kabla ya kufika viwanjani.
 
Pia tunatoa mwito kwa shabiki ambaye atamuona mwenzake akiwa na silaha uwanja kutoa taarifa kwa mamlaka husika likiwemo Jeshi la Polisi ili aweze kuchukuliwa hatua.

No comments:

Post a Comment