KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 24, 2013

MANJI AMTOLEA UVIVU BRANDTS



KOCHA Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts hataongezwa mkataba mpya baada ya mkataba wake wa sasa kumalizika, Juni mwakani.

Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha pamoja kati ya uongozi wa Yanga na benchi la ufundi, kilichofanyika juzi usiku kwenye hoteli ya Protea mjini Dar es Salaam.

Katika kikao hicho, uongozi wa Yanga uliwakilishwa na Mwenyekiti, Yussuf Manji, makamu wake, Clement Sanga wakati benchi la ufundi liliwakilishwa na Brandts, msaidizi wake, Fred Felix Minziro na kocha wa makipa, Razak Siwa.

Katika kikao hicho kilichofanyika kuanzia saa moja hadi saa sita usiku, ilibainika kuwa, Brandts amekuwa na matatizo kutokana na kutokubali kusikiliza ushauri wa wasaidizi wake.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zimeeleza kuwa, Minziro aliamua kueleza bayana kuwa, Brandts amekuwa akimtolea majibu ya kijeuri kila anapompa ushauri na kukataa kumsikiliza.

"Viongozi walimweleza Brandts kwamba, makosa ambayo amekuwa akiyafanya katika kila mechi ni yale yale, hataki ushauri na amekuwa akitoa lugha chafu kwa Minziro na meneja wa timu," kimeeleza chanzo cha habari.

Imeelezwa kuwa, katika mechi ya ligi kuu dhidi ya Simba iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Brandts alikataa kusikiliza ushauri wa meneja wa timu hiyo wa kumwacha Hamisi Kiiza aendelee na mchezo.

"Hafidhi alimshauri asimtoe Kiiza kwa sababu ameshafunga mabao matatu katika ligi na angeweza kuongeza mengine na alikuwa mwiba kwa mabeki wa Simba, lakini alimjibu kijeuri na kuukataa ushauri wake," kilieleza chanzo cha habari.

Katika mechi hiyo, timu hizo kongwe nchini zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya mabao 3-3. Yanga ilikuwa ya kwanza kupata mabao matatu hadi mapumziko, kabla ya Simba kusawazisha kipindi cha pili.

Chanzo hicho cha habari kiliongeza kuwa, kwa vile mkataba wa kocha huyo utamalizika mwishoni mwa ligi hii, uongozi umeamua kutomuongezea mkataba mpya. Pia umemtaka ajirekebishe katika mechi zilizosalia za ligi hiyo, vinginevyo atatimuliwa.

Katika kikao hicho, uongozi wa Yanga pia ulimuonya Siwa kutokana na kiwango cha kipa Ally Mustapha 'Barthez' kushuka, ambapo ameshafungwa mabao 12, tofauti na msimu uliopita, ambapo alimaliza ligi akiwa amefungwa mabao manne.

No comments:

Post a Comment