'
Thursday, October 24, 2013
YANGA YACHINJA, SIMBA YABANWA
MSHAMBULIAJI Hamisi Kiiza jana aling'ara baada ya kuifungia Yanga mabao mawili, ilipoibwaga Rhino Rangers mabao 3-0 katika mechi ya ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kiiza alifunga mabao hayo dakika ya 12 na 81 kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Mrisho Ngasa, ambaye pia alitengeneza bao la tatu lililofungwa na Frank Domayo dakika ya 73.
Ushindi huo umeifanya Yanga iendelee kushika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 19 baada ya kucheza mechi 10. Rhino Rangers inaendelea kushika nafasi ya 11 ikiwa na pointi saba.
Katika mechi hiyo, Yanga iliwapumzisha beki Nadir Haroub 'Cannavaro', kiungo Athumani Iddi 'Chuji' na mshambuliaji Didier Kavumbagu, waliocheza dhidi ya Simba mwishoni mwa wiki iliyopita na nafasi zao kuchukuliwa na Rajabu Zahir, Juma Abdul na Simon Msuva.
Iliwachukua Yanga dakika 12 kupata bao la kwanza lililofungwa na Hamisi Kiiza baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Mrisho Ngasa, aliyetoa pasi kwa Simon Msuva, aliyemimina krosi, ambayo mabeki wa Rhino Rangers walishindwa kuiokoa, mpira ukamkuta mfungaji, aliyeukwamisha wavuni.
Rhino Rangers haikufanya shambulizi kubwa kwenye lango la Yanga katika kipindi cha kwanza, kutokana na safu yake ya ushambuliaji kushindwa kuelewana vyema na ile ya kiungo. Timu hizo zilikwenda mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Vijana hao wa JWTZ walipata nafasi nzuri ya kufunga bao dakika ya 55 wakati mshambuliaji wake, Victor Hangaya alipoingia na mpira ndani ya mita 18, lakini shuti lake lilikuwa mboga kwa kipa Deogratius Munishi 'Dida'.
Baada ya Kiiza kukosa bao lingine dakika ya 72, Frank Domayo alirekebisha makosa dakika moja baadaye kwa kuifungia Yanga bao la pili, kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Ngasa, aliyewahadaa mabeki wawili wa Rhino Rangers.
Bao la tatu la Yanga lilifungwa na Kiiza dakika ya 81, baada ya Ngasa kumtoka Nurdin Bakari pembeni ya uwanja na kutoa pasi kwa mfungaji, aliyeukwamisha mpira wavuni.
Sophia Wakati ameripoti kutoka Tanga kuwa, Simba na Coastal zimeshindwa kutambiana baada ya kutoka suluhu katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Sare hiyo iliiwezesha Simba kurejea kwenye uongozi wa ligi hiyo kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kati yake na Azam na Mbeya City, kufuatia kila moja kuwa na pointi 20 baada ya kucheza mechi 10.
Timu zote mbili zilicheza kwa uangalifu kipindi cha kwanza na kufanya mashambulizi machache ya kushtukiza, lakini hakuna iliyoweza kupata bao.
Simba: Abel Dhaira/ Abuu Hashim, Nassoro Masoud 'Cholo'/Edward Christopher, Haruna Shamte, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhani Singano, Saidi Ndemla, Hamisi Tambwe, Amri Kiemba/Zahoro Pazi, William Lucian 'Galas'.
Coastal Union: Shabani Kado,Mbwana Hamisi, Tamim Othman, Marcus Rafael, Juma Nyoso, Jerry Santo, Daniel Lianga/ Uhuru Selemani, Christopher Odula, Yaiyo Lituma, Haruna Moshi 'Boban', Kenneth Masumbuko.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment