KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, October 21, 2013

SIMBA, YANGA ZAINGIZA MIL 500/-


Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ya watani wa jadi Simba na Yanga iliyochezwa jana (Oktoba 20 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya mabao 3-3 imeingiza sh. 500,727,000.

Washabiki 57,422 ndiyo waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo namba 63 kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.

Ni tiketi 131 tu ndizo hazikuuzwa ambazo ni 90 za VIP A, 40 za VIP B na moja ya VIP C. Tiketi zilizochapwa kwa ajili ya mechi hiyo ni 57,558 ambayo ndiyo idadi ya viti vilivyopo kwenye uwanja huo.

Kila klabu imepata mgawo wa sh. 123,025,564.32 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 76,382,084.75.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 62,555,371.69, tiketi sh. 7,309,104, gharama za mechi sh. 37,533,223.01, Kamati ya Ligi sh. 37,533,223.01, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 18,766,611.51 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 14,596,253.39.


VITAMBULISHO MICHUANO YA CHALENJI
Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limefungua maombi ya vitambulisho (Accreditation) kwa ajili ya waandishi wa habari wanaotarajia kuripoti mashindano ya Kombe la Chalenji.

Mashindano ya Kombe la Chalenji yatafanyika nchini Kenya kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 12 mwaka huu. Kwa waandishi wa habari wanaotaka kuripoti mashindano hayo wanatakiwa kutuma maombi yao kabla ya Oktoba 31 mwaka huu.

Mbali ya majina, katika maombi hayo mwandishi wa habari ni lazima aoneshe chombo anachofanyia kazi na kuambatanisha na picha moja ya pasipoti.

No comments:

Post a Comment