KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, October 20, 2013

BRANDTS: MECHI ITAKUWA NGUMU, LAKINI TUTASHINDA



KOCHA Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts amesema anafurahia timu yake kuweka kambi Pemba kwa ajili ya kuikabili Simba kwa vile hali ya hewa ni nzuri na kuna hali ya utulivu.

Brandts amesema hali hiyo ya utulivu ni miongoni mwa vitu vinavyoweza kuwaongezea wachezaji chachu ya ushindi katika pambano lao dhidi ya Simba.

Kocha huyo kutoka Uholanzi, alisema hayo juzi baada ya timu hiyo kuwasili  Dar es Salaam, ikitokea Pemba kwa ajili ya pambano hilo.

Simba na Yanga zinatarajiwa kushuka dimbani leo katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi kuu, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

"Pemba ni sehemu nzuri, tulikuwepo huku mwishoni mwa msimu uliopita kwa ajili ya maandalizi dhidi ya Simba na tuliibuka na ushindi wa mabao 2-0,"alisema Brandts.

"Uwanja wa mazoezi ni mzuri na hali ya hewa ni nzuri. Naamini vitu hivi vitatuongezea chachu ya ushindi kwa kuwa tupo sehemu tulivu," aliongeza kocha huyo, aliyeanza kuinoa Yanga msimu uliopita.

Brandts alisema anatambua kuwa, pambano lao dhidi ya Simba litakuwa gumu kutokana na ushindani uliopo kati ya timu hizo mbili, lakini amekiandaa kikosi chake kwa lengo la kuibuka na ushindi.

"Tunachotaka ni kuendeleza wimbi la ushindi kwa Simba na pia kutwaa uongozi wa ligi kuu,"alisema kocha huyo.

Vigogo hivyo vya soka nchini, vilikutana kwa mara ya mwisho Mei 18 mwaka huu katika mechi ya marudiano ya ligi hiyo, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Yanga imewasili Pemba ikiwa na msafara wa watu 38, wakiwemo wachezaji wote 29 waliosajiliwa msimu huu na viongozi tisa. Mabingwa hao wataweka kambi Pemba kwa wiki moja.

Baada ya kuwasili Pemba kwa ndege tatu ndogo za kukodi, kikosi cha timu hiyo kilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Gombani kuanzia saa sita mchana na kuendelea tena juzi na jana.

Wachezaji walioweka kambi Pemba ni makipa Ally Mustapha 'Barthez', Deogratius Munishi 'Dida' na Yusuph Abdul. Walinzi wa pembeni ni Mbuyu Twite, Juma Abdul, Issa Ngao, David Luhende na Oscar Joshua.

Walinzi wa kati ni Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani 'Cotton', Rajab Zahir na Ibrahim Job. Viungo wa ulinzi ni Athuman Idd 'Chuji', Frank Domayo, Salum Telela na Bakari Masoud.
Viungo washambuliaji ni Haruna Niyonzima, Nizar Khalfani na Hamis Thabit.

Washambuliaji wa pembeni ni Mrisho Ngassa, Saimon Msuva na Abdallah Mguhi 'Messi'. Washambuliaji ni Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza, Jerson Tegete, Hussein Javu, Said Bahanuzi, Reliants Lusajo na Shaban Kondo

No comments:

Post a Comment