RAIS wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) anayemaliza muda wake, Leodegar Tenga usiku wa
kuamkia leo amemtangaza rasmi Jamal Malinzi kuwa rais mpya wa Shirikisho hilo
baada ya kushinda uchaguzi wa rais wa TFF kwenye Ukumbi wa NSSF Waterfront, Dar
es Salaam.
Kwa mujibu
wa matokeo yaliyotangazwa, Malinzi alipata kura 73, huku mpinzani wake pekee
Athuman Nyamlani akiambulia kura 52. Hii ni tofauti ya kura 21 kati ya mshindi
Malinzi na Nyamlani.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Uchaguzi, Hamidu Mbwezeleni ndiye aliyetangaza matokeo hayo na
kuamsha shangwe ukumbini hapo huku wapambe wa wagombe wengine wakitoka vichwa
chini.
Awali
kabla ya uchaguzi huo, Nyamlani ndiye aliyekuwa Makamu wa rais wa
TFF.
Kwa upande
wa makamu wa rais wa TFF, aliyeshinda ni Wallace Karia aliyepata kura 67,
akifuatiwa na Ramadhan Nasib aliyepata kura 52 na Iman Madega aliyepata kura 6
tu.
Kabla ya
uchaguzi huo, Karia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi inayoendesha Ligi
Kuu ya Bara na Ligi Daraja la Kwanza.
KIDAU, MGOYI,
KABURU, NYENZI WASHINDA UJUMBE
Katika
uchaguzi wa wajumbe wa kamati ya utendaji, Wilfred Kidau alishinda kwa upande wa
kanda ya Dar es Salaam akiwabwaga Alex Crispine Kamuzelya, Muhsin Said Balhabou
na Omary Isack Abdulkadir. Aliyeshinda kanda ya Pwani na Morogoro ni Geofrey
Nyange ‘Kaburu’ aliyewabwaga Farid Nahdi, Juma Abbas Pinto, Riziki Juma Majala
na Twahil Twaha Njoki.
Khalid
Mohamed ameshinda ujumbe kanda ya Tanga, Kilimanjaro akimshinda Davis Elisa
Mosha. Naye Msafiri Mgoyi ameshinda kanda ya Tabora na Kigoma akimshinda Yusuf
Hamis Kitumbo. Ayoub Nyenzi ameshinda kwa upande wa Iringa na Mbeya akiwashinda
David Lugenge, John Exavery Kiteve, na Elias Mwanjala.
Kwa upande
wa Ruvuma na Njombe aliyeshinda ni James Mhagama aliyemshinda Stanley William
Lugenge. Naye Athuman Kambi ameshinda kanda ya Lindi na Mtwara akiwashinda
Francis Kumba Ndulane na Zafarani Mzee Damoder. Na Blassy Kiondo ameshinda kanda
ya Katavi, Rukwa akimbwaga Ayubu Nyaulingo.
IMETOLEWA KWENYE BLOGU YA SHAFFIH DAUDA
No comments:
Post a Comment