KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 3, 2013

JULIO; KASEJA BADO BONGE LA KIPA

 

KOCHA Msaidizi wa timu ya soka ya Simba, Jamhuri Kihwelo 'Julio' amesema bado anaamini kuwa, nahodha wa zamani wa timu hiyo, Juma Kaseja ndiye kipa bora nchini kwa sasa.

Julio alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, hakuna kipa anayeweza kufikia uwezo wa Kaseja kwa sasa ni kwamba watu wasiokubali ukweli huo, wanalo jambo kwenye mioyo yao.

"Kuna watu wanaomkataa Mwenyezi Mungu licha ya ukweli kwamba ndiye aliyetuumba, vivyo hivyo wapo wanaompinga Kaseja kwa sababu zao, lakini kwangu mimi Kaseja bado kipa bora nchini kwa sasa,"amesema Julio.

Julio alieleza kusikitishwa kwake na taarifa kuwa, wapo watu waliopeleka taarifa mbaya kwa klabu ya FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuhusu Kaseja ili isimsajili msimu huu.

Amesema watu waliotoa taarifa hiyo kwa FC Lupopo hawamtakii mema kipa huyo na kwamba wana roho mbaya na hawataki afike mbali kimaendeleo.
                                                           ROHO MBAYA
Julio amesema moja ya sababu zinazokwamisha maendeleo ya soka nchini ni baadhi ya watu kupenda kufitiniana na kujengeana chuki bila sababu za msingi na wengine kutofurahia maendeleo ya wenzao.

"Tanzania itapata mafanikio katika soka na michezo mingine, iwapo kizazi cha sasa kitatoweka. Pengine kizazi kijacho ndicho kitakacholeta mabadiliko,"amesema mchezaji huyo wa zamani wa Simba na timu ya Taifa, Taifa Stars.

Julio amesema tabia ya wivu na roho mbaya miongoni mwa wadau wa soka nchini, ndiyo iliyomfanya aamue kuwapaleka watoto wake kwenye shule ya soka iliyoko Arabuni.

Amesema awali, aliwapeleka watoto wake hao Arabuni kwa msaada wa mfanyabiashara marehemu Isihaka Kibene na baada ya kuonyesha maajabu, wamepata nafasi katika shule moja iliyoko katika mji wa Abu Dhabi.

Julio amesema watoto wake hao, Super na Kihwelo, ambao wamemaliza kidato cha nne, maendeleo yao ni mazuri na wamemweleza wakala wao kwamba wanataka kwenda kucheza soka ya kulipwa Ulaya.

"Sikupenda niwaingize kwenye timu za Bongo kwa sababu ya wivu na roho mbaya. Wangeweza kuumizwa ama kufanyiwa lolote baya ili kukwamishwa,"amesema beki huyo, ambaye aliwahi kucheza soka ya kulipwa Arabuni kwa zaidi ya miaka saba.
                                                      SHULE ZA SOKA
Kocha huyo ametoa mwito kwa serikali kujenga uwanja mwingine wa kisasa wa soka katika eneo la Jangwani au Tanganyika Packers, Dar es Salaam ili kuongeza hamasa ya mchezo huo.

Julio pia ametoa mwito wa kuanzishwa kwa shule nyingi zaidi za soka kwa lengo la kuibua vipaji vya vijana na kuwaendeleza. Amesema Tanzania inayo hazina ya vijana wengi wenye vipaji vya kucheza soka, lakini kinachokosekana njia za kuwaibua na kuwaendeleza.

Kocha huyo mwenye makeke hakuwa tayari kueleza matumaini ya Simba katika msimu huu wa ligi kwa madai kuwa ni mapema kufanya hivyo kwa kuwa ligi ndiyo kwanza imeanza.

Vilevile alikataa kueleza matumaini ya timu yake katika mechi yao dhidi ya watani wa jadi Yanga, itakayopigwa Oktoba 20 mwaka huu kwa madai kuwa, mechi kati yao huwa hazitabiriki.

                                                        BONGO MOVI
Julio amewataka wasanii wa filamu na muziki wa kizazi kipya nchini, kujenga uhusiano wa karibu na wanamichezo badala ya kujiona wapo juu kuliko wenzao.

Amesema amekuwa akisitishwa na tabia ya wasanii wa Bongo Movi kushindwa kutoa ushirikiano kwa wanamichezo, hasa wakati wa misiba kwa kujiona wapo matawi ya juu.

"Sisi wanamichezo tulishiriki vizuri katika msiba wa marehemu Steven Kanumba, lakini  wakati wa msiba wa marehemu Patrick Mafisango, hakuna mcheza filamu hata mmoja aliyeonekana msibani," alisema.

Julio ni mtoto wa pili katika familia ya watoto tisa ya marehemu Kihwelo. Kwa sasa wamebaki watoto sita baada ya watatu kufariki. Watoto wote wa kiume walikuwa wakijihusisha na soka, wakifuata nyayo za kaka yao, marehemu Mussa Kihwelo.

Alianza kucheza soka katika kikosi cha Simba Kids miaka ya 1980 kabla ya kupandishwa kikosi cha Simba B na baadaye timu ya wakubwa, ambayo aliichezea kwa miaka 11. Pia aliichezea Taifa Stars kwa miaka sita.

No comments:

Post a Comment