KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, October 20, 2013

SIMBA, YANGA HATUMWI MTOTO DUKANI LEO

Haruna Niyonzima
Joseph Owino
Athumani Iddi
Betram Mwombeki

TIMU kongwe za soka nchini, Simba na Yanga zinatarajiwa kushuka dimbani leo katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pambano hilo litakuwa la kwanza kuzikutanisha timu hizo mbili zenye utani wa jadi wa soka nchini. Msimu uliopita, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya kwanza ya ligi iliyochezwa Oktoba 3, 2012 kwenye uwanja huo na ziliporudiana Mei 18 mwaka huu, Yanga iliichapa Simba mabao 2-0.

Kwa kawaida, pambano hilo hutawaliwa na majigambo mengi kutoka kwa viongozi, wanachama na mashabiki wa klabu hizo. Ni mechi ya kutafuta heshima zaidi, hasa ikizingatiwa kuwa, hakuna timu inayopenda kufungwa na mtani wake.

Yanga, inayonolewa na Kocha Ernie Brandts kutoka Uholanzi, iliondoka mjini Dar es Salaam, Jumatatu iliyopita kwenda Pemba kuweka kambi kwa ajili ya kujiandaa kwa pambano hilo. Timu hiyo ilikwenda Pemba kwa ndege tatu za kukodi, ikiwa na kikosi cha wachezaji 28 na viongozi wawili.

Mabingwa hao watetezi, wamekuwa wakifanya mazoezi mara mbili kwa siku kwenye Uwanja wa Gombani na uongozi umewaahidi wachezaji mamilioni ya pesa iwapo watashinda pambano hilo.

Simba imeweka kambi kwenye hoteli ya Bamba Beach, iliyoko Kigamboni, nje ya Jiji la Dar es Salaam. Timu hiyo inanolewa na Kocha Abdalla Kibadeni, akisaidiwa na Jamhuri Kihwelo 'Julio'.

Timu hizo zitashuka dimbani huku Yanga ikiwa na kikosi kile kile cha msimu uliopita wakati Simba inaundwa na wachezaji wengi wapya, wakiwemo nyota wanne wa kulipwa.

Mchezaji pekee aliyeongezeka kwenye kikosi cha Yanga ni mshambuliaji Mrisho Ngasa, ambaye msimu uliopita aliichezea Simba. Itakuwa mechi ya kwanza kwa Ngasa kuichezea Yanga dhidi ya Simba baada ya miaka mitatu.

Wachezaji wapya wa Simba wanaotarajiwa kushuka dimbani kwa mara ya kwanza Jumapili ni kipa Abel Dhaira, beki Gilbert Kaze, mshambuliaji Hamisi Tambwe kutoka Burundi na Betram Mombeki.

Katika mechi hiyo, Simba itawakosa kipa wake wa zamani, Juma Kaseja na mshambuliaji Felix Sunzu kutoka Zambia, ambao mikataba yao imemalizika. Wengine watakaokosekana ni beki Shomari Kapombe, aliyetimkia Ufaransa, Mwinyi Kazimoto, aliyeko Qatar na Mussa Mude, ambaye ameachwa kwenye usajili.

Simba itashuka dimbani huku ikiwa inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 18 baada ya kucheza mechi nane wakati Yanga ni ya nne ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza idadi hiyo ya mechi.

Katika mechi hizo nane, Simba imeshinda mechi tano, imetoka sare tatu, imefunga mabao 17 na kufungwa matano. Yanga imeshinda mechi nne, imetoka sare tatu, imefungwa moja, imefunga mabao 15 na kufungwa manane.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya soka nchini wamekuwa wakiipa Yanga nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi dhidi ya Simba kutokana na kuundwa na wachezaji wengi mahiri na waliokaa pamoja kwa muda mrefu ikilinganishwa na wapinzani wao.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi hao na makocha wa timu zinazoshiriki ligi kuu, wamekiri kuwa, kwa kawaida pambano la Simba na Yanga huwa halitabiriki na timu nzuri inaweza kufungwa na timu mbovu.

Kocha Mkuu wa Azam, Stewart Hall ameipa Yanga asilimia 90 ya kuibuka na ushindi katika pambano hilo huku akiipa Simba asilimia 10.

“Bila kuficha, ukiniuliza nani ataibuka na ushindi Jumapili, bila wasiwasi nitakwambia asilimia 90 Yanga itashinda, Simba ina asimilia 10 tu,"alisema Hall alipokuwa akizungumzia pambano hilo wiki hii.

“Unajua kwanini? Yanga ina wachezaji bora zaidi, lakini kubwa ni kwamba wamekaa pamoja kwa muda mrefu tofauti na Simba, ambayo ndiyo kwanza inajengwa hivyo inahitaji muda,” aliongeza kocha huyo kutoka Uingereza.

Hall alitoa mfano wa mabeki wawili wa kati wa Yanga, Kevin Yondani na Nadir Haroub 'Cannavaro' kwamba wana uzoefu mkubwa na wamekaa pamoja kwa muda mrefu.

Kocha huyo alimwelezea beki wa pembeni, David Luhende kuwa ni kijana mdogo, lakini amepevuka huku akimsifia Mbuyu Twite kwamba ni mchezaji mwenye kiwango bora.

Hall alisema pia kuwa, safu ya kiungo ya Yanga inaundwa na wachezaji wenye uzoefu, akiwataja Haruna Niyonzima na Athumani Iddi 'Chuji', ikilinganishwa na Simba, ambayo inamtegemea zaidi Jonas Mkude na Henry Joseph, ambao hawajacheza pamoja kwa muda mrefu.

"Nimezitazama timu hizi msimu huu mara mbili kila moja, hivyo nimebaini uzuri na upungufu wao,"alisisitiza Hall.

“Ukiwatazama mabeki wawili wa kati wa Simba, utagundua bado hawajazoeana sawasawa kama wale wa Yanga, kwa kifupi Simba ya sasa ni kama Azam yangu, kuna vijana wadogo wazuri, lakini wanatakiwa kujifunza polepole kabla ya kuwa wachezaji wa kutegemewa,”aliongeza.

Kocha Mkuu wa JKT Ruvu, Mbwana Makata amekisifu kikosi cha Simba kwa kusema kuwa, kutokana na kuundwa na vijana wengi wadogo, wanacheza kwa kasi muda wote wa mchezo.
Makata alisema anaamini iwapo Kocha Mkuu wa Simba, Kibaneni atapewa muda zaidi wa kukinoa kikosi hicho, kitakuwa tishio katika ligi kuu msimu ujao

"Simba ni wazuri sana, nimecheza nao na kugundua kwamba wana kikosi imara.
Yanga nao sio wabaya, lakini nimeona kama bado kidogo wana kasoro kwenye sehemu ya ushambuliaji, wanapoteza nafasi nyingi za kufunga mabao na wakati mwingine ngome yao inakatika wakati wakishambuliwa na kuruhusu mabao ya kizembe,"alisema Makata.

Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa, amekiri kwamba timu hizo zinaundwa na wachezaji wengi wazuri, lakini hakuwa tayari kubashiri matokeo ya mechi kati yao.

Hata hivyo, Mkwasa amesema timu hizo bado zina matatizo makubwa kwenye safu zake za ushambuliaji kutokana na washambuliaji wake kutokuwa makini katika kufunga mabao.

Mkwasa alisema pambano kati ya watani hao wa jadi litakuwa na ushindani mkali na timu yoyote inaweza kushinda. Alisema mara nyingi matokeo ya mechi kati ya Simba na Yanga hayategemei ubora wa timu.

Kocha Mkuu wa Mbeya City, Juma Mwambusi amesema timu hizo zinaundwa na wachezaji wengi wazuri, na kuongeza kuwa, yoyote inaweza kushinda pambano la Jumapili.

Hata hivyo, Mwambusi anapinga sera za timu hizo kusajili wachezaji kutoka nje kwa madai kuwa, zimepitwa na wakati. Amesema Tanzania inayo hazina kubwa ya wachezaji wenye vipaji vya kucheza soka

Makocha wasaidizi wa Simba na Yanga, Jamhuri Kihwelo na Fred Felix Minziro kila mmoja amekuwa akitamba kuwa, timu yake itaibuka na ushindi katika mechi hiyo na kutoka uwanjani na pointi zote tatu.

Minziro alikaririwa na vyombo vya habari wiki hii akisema kuwa, timu yake imekamilika katika kila idara na kuongeza kuwa, majigambo ya Julio yamewafanya wachezaji wake wawe na ghadhabu ya kushinda mechi hiyo.

Kocha huyo, ambaye ni mchezaji wa zamani wa Yanga, alikwenda mbali zaidi kwa kuapa kuwa, iwapo watafungwa mechi hiyo na Simba, watavunja timu kwa vile haitakuwa na kitu kipya na cha kujivunia.

Minziro alisema wamekuwa wakifanya mazoezi ya nguvu ili kila mchezaji awe fiti na pia waweze kutoa kipigo kikubwa kwa wapinzani wao, ambacho kinaweza kuwafanya wachanganyikiwe.

Katika miaka ya hivi karibuni, Simba ndiyo yenye rekodi ya kutoa kipigo kikubwa kwa Yanga baada ya kuitandika mabao 5-0 katika mechi ya ligi kuu, iliyochezwa mwaka 2012 kwenye uwanja huo.

Kwa upande wake, Julio alisema Yanga haina uwezo wa kuifunga Simba, licha ya timu yake kuundwa na wachezaji wengi wapya na wenye umri mdogo.

Kocha huyo, ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars alisema, wamepania kutoa kipigo kwa Yanga ili kuwaonyesha kuwa, timu yao ni bora na ndio sababu inaongoza ligi.

Burudani murua katika pambano hilo inatarajiwa kujitokeza kwa mabeki Yondani na Cannavaro dhidi ya Tambwe na Mombeki na ile kati ya Mbuyu na Haruna Chanongo. Nyingine itakuwa kati ya Niyonzima na Mkude, Henry na Chuji, Joseph Owino na Didier Kavumbagu, Hamisi Kiiza na Kaze, Idrisa Rashid na Ngasa.

No comments:

Post a Comment