KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, May 25, 2014

MBEYA CITY YAANZA VIZURI KOMBE LA NILE BASIN



WAWAKILISHI wa Tanzania Bara katika michuano mipya ya klabu ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) iitwayo Nile Basin, Mbeya City wameanza vizuri leo baada ya kuifunga mabao 3-2 Academie Tchite ya Burundi mjini Khartoum, Sudan.


Mabao ya Mbeya City katika mchezo huo wa Kundi B yamefungwa na Paul Nonga dakika ya 15, mshambuliaji mpya Themi Felix kutoka Kagera Sugar dakika ya 27 na Mwagane Yeya dakika ya 37. Mabao ya timu ya Burundi yamefungwa na Rashid Patient dakika ya 10 na Munirakiza Cedric dakika ya 68.

Ushindi huo unawaweka Mbeya City katika nafasi nzuri ya kutinga Robo Fainali ya michuano hiyo.

Mapema katika mechi za ufunguzi jana, mabao saba yalitinga nyavuni, Victoria University ya Uganda ikiilaza 1-0 Malakia ya Sudan Kusini, El-Merreikh waliichapa 3-0 Polisi ya Zanzibar na El-Shandi waliilaza 2-1 Dkhill ya Djibouti.

Michuano hiyo inashirikisha mabingwa wa Kombe la FA na washindi wa pili wa Ligi Kuu wa nchi wanachama wa CECAFA. Mbeya City imechukua nafasi ya Azam FC, washindi wa pili wa Ligi Kuu msimu uliopita, ambao wamejitoa.

Simba SC ambao wangechukua nafasi ya Azam, wakati taarifa inakuja ya kufanyika kwa mara ya kwanza michuano hiyo, walikuwa wamekwishavunja kambi na wachezaji wao wote walikuwa wameruhusiwa likizo.

No comments:

Post a Comment