KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, May 18, 2014

MWILI WA AMINA NGALUMA KUREJESHWA NCHINI KWA MAZIKO

 
MWILI wa mwanamuziki Amina Ngaluma 'Japanese Girl' aliyefariki dunia nchini Thailand wiki iliyopita, huenda ukarejeshwa nchini kwa ajili ya kufanyiwa maziko wiki ijayo.

Amina ni mwanamuziki wa zamani wa bendi za African Revolution 'Tamtam' na Double M Sound, zilizokuwa zikiongozwa na Muumin Mwinjuma.

Hadi mauti yalipomkumba, Amina alikuwa akiimbia bendi ya Jambo Survivors iliyokuwa na mkataba wa miaka minne nchini Thailand, akiwa na akina Ramadhani Kinguti na Hassan Show.

Habari za uhakika kutoka Thailand zimeeleza kuwa, Amina alifariki akiwa hospitali, ambako alilazwa kwa ajili ya kufanyiwa operesheni ya kichwa.

Mume wa marehemu, Rashid Sumuni, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wameshaanza kufanya maandalizi ya kuurejesha mwili wa marehemu nchini.

"Tunasubiri taratibu za kuurejesha mwili kutoka Thailand. Kwa sasa tunafanya mipango ya kutafuta nyaraka kutoka ubalozi wa Tanzania nchini Singapore kwa vile hatuna ubalozi Thailand,"alisema Sumuni.

Sumuni, ambaye ni mmoja wa wapiga gita hodari la solo nchini, alisema awali alipata taarifa kutoka kwa kiongozi wa Jambo Survivors kuhusu kuugua kwa mkewe na kwamba walimpeleka hospitali kupatiwa matibabu.

Aliongeza kuwa, alizungumza na Amina kwa mara ya mwisho Alhamisi iliyopita na kumuahidi kwamba angempigia simu Jumamosi kumpa maelekezo fulani, ambayo hakuweza kuyajua.

Sumuni alidokeza pia kuwa, katika mazungumzo hayo, Amina alimwelezea kuhusu hali ya kutokuelewana iliyojitokeza kati yake na wanamuziki wenzake wa bendi hiyo.

"Aliniambia kuna mambo walikuwa hawaelewani lakini nilimpa moyo na kumtaka afanyekazi,"alisema.

Kwa mujibu wa Sumuni, yeye na mkewe walipanga kuendeleza maisha yao hapa nchini baada ya Amina kumaliza mkataba wake na bendi ya Jambo.

Licha ya kuishi mbali na mkewe, Sumuni alisema walikuwa wakipendana na kuheshimiana.

No comments:

Post a Comment