KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, September 4, 2017

BODI YA WADHAMINI TFF YAKUTANA NA UONGOZI MPYA



Bodi ya Wadhamini wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, imekutana na viongozi wakuu wa Shirikisho katika Ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Sea Scape, Kunduchi, Dar es Salaam.

Bodi hiyo imekutana na uongozi wakuu wa TFF jana Septemba 2, mwaka huu kwa mara ya kwanza tangu ithibitishwe na Mkutano Mkuu wa TFF.

Madhumuni ya Bodi hiyo kukutana na viongozi wa TFF  - Rais Wallace Karia; Makamu wa Rais, Michael Wambura na Kaimu Katibu Mkuu, Kidao Wilfred ni kufahamiana.

Kwa upande wa Bodi walikuwa Mhe. Mohammed Abdulaziz, Mhe. Balozi Dk. Ramadhani Dau, Mhe. Abdallah Bulembo na Mhe. Stephen Mashishanga. Mjumbe Dk. Joel Bendera hakuhudhuria kwa udhuru.

Kadhalika Bodi hiyo kwa mujibu wa katiba ya TFF, walipata nafasi ya kuchagua Mwenyekiti wa Bodi ambako Mhe. Mohammed Abdulaziz alichaguliwa kushika wadhifa huo. Mhe. Abdulaziz alikuwa Mlezi wa timu ya Daraja la Kwanza ya Kariakoo ya Lindi

Kwa niaba ya Wajumbe wa Bodi, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhe. Mohammed Abdulaziz ambaye ni Mbunge wa zamani wa Jimbo la Lindi Mjini, aliupongeza uongozi mpya wa TFF ulioingia madarakani Agosti 12, mwaka huu akisema: “Mmeanza vizuri.”

Kadhalika Mwenyekiti ambaye alipata kuwa Mkuu wa Mikoa ya Tabora, Tanga na Iringa kwa nyakati tofauti , aliahidi ushirikiano kwa uongozi wa TFF ambako kwa upande wa TFF, Rais Karia alipokea pongezi hizo na baraka tele za kuanza vema na ushirikiano.

Mhe. Balozi Dk. Dau - alikuwa Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ni mwanafamilia ya mpira wa miguu aliyejitolea hata kwa nguvu zake binafsi kusaka vipaji vya mpira wa miguu kwa vijana.

Mhe. Joel Bendera ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara. Ni Kocha wa zamani wa timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ aliyekuwa na mchango mkubwa kuifikisha kucheza fainali za Kombe la Mataifa Huru ya Afrika (CAN 1980) sasa michuano hiyo inafamika kwa jina la AFCON. Fainali za mwaka 1980 zilifanyika Lagos, Nigeria.

Mhe. Stephen Mashishanga ni Mkuu wa zamani wa Morogoro mwenye historia nzuri ya unafamilia wa mpira wa miguu akitoa mchango mkubwa katika maendeleo tangu alipokuwa kiongozi hadi sasa. Pia alipata kuwa Mlezi wa timu ya Milambo ya Tabora iliyoshiriki Ligi Kuu Bara.

Mhe. Abdallah Bulembo ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyepata kuwa Makamu Mwenyekiti wa kilichokuwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT).

No comments:

Post a Comment