KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, September 11, 2017

WITNESS: NAJIVUNIA NA KUUTHAMINI UTANZANIA WANGU






MSHINDI wa taji la Miss Garden Route 2017/2018, lililoshindaniwa nchini Afrika Kusini, Witness Kavumo, amesema anaona fahari na kujivunia kuwa Mtanzania na pia kuonyesha uzalendo kwa nchi yake.

Amesema licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi kwa muda wote aliokuwa akisoma Afrika Kusini, ikiwemo ubaguzi wa rangi, amekuwa akikabiliana nazo kwa kujivunia rangi yake na utaifa wake.

Witness (21), amesema katika shindano hilo lililoandaliwa na Kampuni ya The Role Models Foundation, ikishirikiana na Gemini Modelling Agency', alikuwa mshiriki pekee mweusi. Shindano hilo liliwashirikisha mabinti 600 katika hatua za awali.

Amesema baada ya mchujo wa awali, alikuwa miongoni mwa warembo 12, waliotinga fainali na hatimaye kuibuka mshindi, ambapo alizawadiwa Randi 4,000 za Afrika Kusini, sawa na sh. 640,000.

Shindano hilo, ambalo washiriki wengi walikuwa wazungu, lilifanyika Mei 6, mwaka huu, katika mji wa George, Afrika Kusini.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, hivi karibuni, Witness alisema alikwenda Afrika Kusini kwa ajili ya masomo, lakini alipenda kutumia muda wake wa ziada kujihusisha na masuala ya urembo.

Binti huyo mzaliwa wa mkoa wa Arusha, amesema washindani katika hatua ya mwisho waliwapa wakati mgumu majaji kutokana na kuwa na mvuto na uchangamfu, lakini hatimaye aliibuka mshindi.

Licha ya kuwa ugenini, Witness anasema alishiriki katika shindano hilo akijitambulisha kuwa ni Mtanzania na baada ya kushinda, ameamua kuja kujitambulisha katika Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo ili serikali imtambue.

"Nilikutana na vikwazo vingi, ikiwemo ubaguzi wa rangi na kukosa ushirikiano hata kwa Watanzania wenzangu, lakini nilikabiliana navyo na hatimaye nikaibuka mshindi," amesema binti huyo anayezungumza kwa kujiamini.

Amewataka wanawake wenzake kusimama imara, kujiamini na kukabiliana na vikwazo vyote wanavyokumbana navyo katika maisha, bila kujali wapo nyumbani au ugenini kwa sababu hakuna linaloshindikana.

"Nauthamini na kujivunia utanzania wangu ndio sababu nilifanikiwa kushinda," amesema binti huyo.

Witness amesema anawashukuru wazazi wake kwa kumuunga mkono na kumpa moyo wa kushiriki kwenye mashindano mbalimbali ya urembo, yakiwemo ya vyuo vikuu mkoani Arusha, ambapo aliibuka mshindi akiwa na umri wa miaka 18.

Kutokana na kuibuka mshindi wa shindano la Miss Garden Route, Witness amepata mkataba wa kufanyakazi za urembo chini ya udhamini wa kampuni za The Role Models Foundation na Gemini Modelling Agency.

Witness anasema japokuwa zawadi aliyopata kwa kushinda shindano hilo ni ndogo, lakini anajisikia faraja kupata mkataba wa udhamini wa kufanyakazi ya urembo na kampuni hizo mbili za Afrika Kusini.

Akizungumzia ushindi wa binti huyo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura, amewataka vijana nchini kutumia muda vizuri na mazingira yanayowazunguka ili kufikia azma ya malengo waliyojiwekea katika kujiletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Naibu Waziri Anastazia alitoa kauli hiyo alipokuwa akimpongeza Witness, ambaye pia alitambulishwa kwa wabunge, katika moja ya vikao vya bunge vinavyoendelea mjini Dodoma.

“Ni dhahiri umetumia ujuzi, ubunifu, sanaa, imani, bidii, desturi, maadili na sheria, ambavyo umevipata  kutoka kwa familia, jamii ya Kitanzania na pia kwa jamii ya watu wa  Afrika Kusini,” amesema Anastazia.

“Vijana wa Kitanzania, Witness  amewaonesha njia, mjenge utamaduni wa kupambana na mazingira ili kufikia azma mnazojiwekea,” amesisitiza Naibu Waziri.

Aidha, amesema mrembo huyo ameonyesha uzalendo kwa nchi yake, kwa kuamua kwenda Dodoma na kutoa taarifa ya mafanikio yake kama Mtanzania, kutokana na ushindi alioupata katika mashindano hayo ya ubunifu.

Amesema hatua hiyo inaonyesha kuwa Witness ameumeuthamini Utanzania wake na kuonyesha kujali kutumia muda wa ziada katika masuala ya fani ya urembo licha ya kwamba, jukumu lake la msingi nchini humo ni masomo.

Naibu Waziri amesema fani ya ubunifu na mitindo inatambulisha utamaduni, kuongeza kipato, kuinua uchumi na kukuza utalii kwa kuongeza juhudi, maarifa na kufanyakazi kwa bidii, hatua ambayo inaleta matokeo mazuri yenye tija.

Amemshauri Witness, kutumia bidhaa zenye asili ya Tanzania katika fani yake ili kuzitangaza katika soko la ndani na la nje, kuvutia utalii, kuingiza kipato na  kukuza uchumi katika ngazi zote za mnyororo wa thamani katika sekta ya ubunifu wa mavazi na mitindo, kwake yeye binafsi na kwa Taifa.

No comments:

Post a Comment