KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, December 9, 2011

PETER TINO; Mwanasoka aliyeipeleka Stars fainali za Afrika 1980


Peter Tino (kulia) akiwa na mwanasoka mwenzake mkongwe, Kitwana Manara


IKUWA Agosti 26,1979 wakati timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars ilipokuwa ikirudiana na timu ya soka ya Taifa ya Zambia katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 1980 zilizofanyika nchini Nigeria.Pambano hilo lilichezwa mjini Ndola.
Mechi hiyo ilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Taifa Stars kwa vile ilikuwa ikihitaji sare ya aina yeyote ili iweke historia ya kufuzu kucheza fainali hizo kwa mara ya kwanza , tangu ilipoanza kushiriki michuano hiyo mwaka 1968.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa wiki mbili nyuma kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Taifa Stars iliishinda Zambia bao 1-0. Bao hilo lilifungwa na kiungo Mohammed Rishard Adolph.
Ushindi huo ulipatikana kwa mbinde kiasi kwamba mashabiki wengi hawakuwa na imani iwapo Taifa Stars ingeshinda ama kupata sare katika mechi ya marudiano. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwani Wazambia walifanikiwa kupata bao la kuongoza dakika za mapema na kudumu nalo kwa takriban dakika 86.
Zikiwa zimesalia dakika tatu pambano hilo kumalizika, mshambuliaji mrefu mwenye kasi na mashuti makali, Peter Tino alibadili sura ya mchezo na kufanya kile kilichokuwa kikisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa mchezo huo nchini.
Ilipigwa kona kwenye lango la Taifa Stars, kipa Juma Pondamali akaupangua mpira kwa ngumi, ukamkuta kiungo Leodegar Tenga, aliyetoa pasi ndefu kwa kiungo mwenzake, Hussein Ngulungu, ambaye naye alitoa pasi ndefu kwa Tino.
Akiwa amezungukwa na mabeki watatu wa Zambia, Tino alilazimika kupiga hesabu za haraka haraka. Aliwachomoka mbio mabeki nao na kukimbia na mpira kwa kasi. Alipofika nje kidogo ya eneo la hatari la Zambia, alifumua shuti kali la mguu wa kulia, lililompita kipa Shileshi wa Zambia na mpira kutinga wavuni.Bao hilo lilipatikana baada ya pasi tatu.
Katika mechi hiyo, Taifa Stars iliwakilishwa na kipa Juma Pondamali,mabeki ni Leopard Tasso, Mohammed Kajole/ Ahmed Amasha, Salim Amir, Jella Mtagwa, viungo ni Leodegar Tenga, Hussein Ngulungu na washambulaji ni Omari Hussein, Peter Tino, Mohamed Salim na Thuweni Ally.
Kikosi hicho kilichokuwa chini ya Kocha Slowmir Work kutoka Poland, akisaidiwa na Joel Bendera na Ray Gama, ndicho kilichoiwakilisha Tanzania katika fainali za kombe hilo zilizofanyika nchini Nigeria.
Katika fainali hizo, Taifa Stars ilichapwa mabao 3-1 na wenyeji Nigeria katika mechi ya ufunguzi, ilitoka sare ya mabao 2-2 na Ivory Coast kabla ya kuchapwa mabao 2-1 na Misri na kutolewa hatua ya makundi.
Hivi sasa Tino hajihusishi kabisa na masuala ya soka, si kwa kazi ya ukocha wala uongozi. Aliamua kutundika daruga zake ukutani mwishoni mwa miaka ya 1980 akiwa klabu ya Yanga. Alistaafu soka kwa kile alichodai kuwa, mwili wake umechoka na pia alitaka kutoa nafasi kwa wanasoka chipukizi kuonyesha vipaji vyao.
Akizungumzia maendeleo ya soka hivi sasa hapa nchini, Tino alisema ni mazuri hasa ikizingatiwa kuwa, serikali ipo mstari wa mbele kuihudumia timu ya taifa na pia wamejitokeza wafadhili wengi, lakini tatizo lipo kwa wachezaji.
Alisema wanasoka wa Tanzania kwa sasa, kuanzia ngazi ya klabu hadi taifa, hawana upendo miongoni mwao, hawajitunzi, wanabweteka na sifa na wameweka mbele zaidi anasa, tofauti na wachezaji wa zamani.
"Enzi zetu hatukuwa tukibweteka na sifa za wapenzi. Binafsi nimechezea timu ya taifa kwa miaka minane mfululizo kwa sababu nilijitunza na sikuwa nikiendekeza anasa,"alisema.
"Lakini sasa hivi, mchezaji msimu wa kwanza anachezea Yanga, wa pili Simba, mara msimu huu anacheza vizuri, msimu unaofuata anavurunda," aliongeza.
Tino alisema enzi zao, kila walipokuwa wakisifiwa na mashabiki, walijiona kama vile wanadanganywa na bado hawajafika kiwango cha juu, tofauti na hivi sasa, ambapo alidai kuwa, wachezaji huanza kujiona nyota baada ya kucheza soka kwa kipindi kifupi.
Mshambuliaji huyo nyota wa zamani wa klabu za Pan African, African Sports na Yanga alisema, hata mazoezi waliyokuwa wakiyafanya wachezaji wa zamani, ni tofauti na sasa na kwamba, walikuwa na nidhamu ya hali ya juu na waliheshimu makocha na viongozi wao.
"Hivi sasa wapo baadhi ya wachezaji wanawazidi nguvu viongozi na makocha na kuamua wanavyotaka, ndio sababu hata viwango vyao vinashuka haraka. Mchezaji mechi mbili anacheza vizuri, ya tatu kiwango kinashuka," alisema.
Tino alisema maslahi ya wachezaji wa zamani yalikuwa madogo, lakini kwa vile soka ilikuwa kwenye damu yao, walicheza kwa nguvu na kujituma.
Alisema iwapo maslahi wanayopata sasa wachezaji wa Taifa Stars, yangekuwepo enzi zao, Tanzania ingeweza kufuzu kucheza fainali za kombe la Dunia miaka ya 1980.
Akitoa mfano, Tino alisema katika mechi ya mwisho ya michuano ya kucheza fainali za kombe hilo mwaka 1982, Taifa Stars iliilazimisha Nigeria kutoka nayo sare ya bao 1-1 katika mechi ya awali iliyochezwa mjini Lagos. lakini ziliporudiana mjini Dar es Salaam, Taifa Stars ulifungwa mabao 2-0.
"Tulikuwa tukihitaji sare ya bila kufungana ili tufuzu kucheza fainali. Tungekuwa tunapata maslahi mazuri na motisha kama ilivyo sasa, nina hakika tungefuzu kucheza fainali kwani Nigeria wasingetufunga nyumbani,"alisema.
"Hivi sasa Rais Jakaya Kikwete ni mhamasishaji mkuu wa maendeleo ya soka, kampuni nyingi zimejitokeza kuidhamini Taifa Stars na wachezaji wamekuwa wakilipwa mamilioni ya pesa. Enzi zetu ukizungumzia soka, ni wachezaji, chama cha soka na labda waziri mwenye dhamana ya michezo,"aliongeza.
Akizungumzia sababu za kufungwa mara kwa mara kwa Taifa Stars katika mechi za kimataifa zinazochezwa hapa nchini, Tino alisema ni kutokana na matatizo binafsi ya wachezaji.
Tino alisema wanasoka wanaoteuliwa kuichezea Taifa Stars wanashindwa kwenda na kasi ya mchezo, kubadilika kulingana na mchezo unavyoendelea na pia kuondokana na dhana kwamba, kumiliki mpira ndio ushindi.
Mwanasoka huyo mkongwe alisema, kama wachezaji wa Taifa Stars wangekuwa na kawaida ya kuonyesha uwezo wao binafsi, wangeweza kushinda mechi nyingi za kimataifa zinazochezwa hapa nchini.
"Mimi huwa nasikitika sana ninapoona wachezaji wa hapa nchini wanapata huduma nzuri, wanalipwa vizuri, wanaye kocha mzuri, lakini wanakosa juhudi binafsi. Ukibebwa unatakiwa ung'ang'anie," alisisitiza.
Alizitaja kasoro zingine alizozigundua kwa wanasoka wengi wa Tanzania kuwa ni pamoja na kukosa ujanja na mbinu za kimchezo, kutojiamini na kutohamasishana wanapokuwa uwanjani.
Akitoa mfano, Tino alisema mchezaji anaweza kuwa peke yake na mpira, lakini badala ya kuuvuta na kwenda nao mbele, anatoa pasi hovyo kwa kuogopa lawama. Alisema mchezo wa soka ni wa lawama, hivyo wachezaji hawapaswi kuziogopa.
"Ni nadra hivi sasa kuwapata washambuliaji wajanja wajanja kama ilivyokuwa kwa Zamoyoni Mogella, Issa Athumani, Saidi Suedi na wengineo. Vilevile ni nadra kuwakuta wachezaji wakihamasishana uwanjani. Enzi zetu tulikuwa tunaongea kwa kustuana. Hivi sasa, vijana wetu wanacheza kama mabubu," alisema.
Tino alisema kama enzi zao kungekuwepo na televisheni, wachezaji wa sasa wangeweza kujifunza mengi kutoka kwao na kupata akili kuhusu soka.
Mshambuliaji huyo mkongwe pia alieleza kushangazwa kwake na maumbile ya wachezaji wa sasa, ambayo alisema ni tofauti na yale waliyokuwa nayo wachezaji wa zamani. Alisema enzi zao walikuwepo wachezaji wafupi kama vile Omari Hussein na Shaaban Katwila, lakini walikuwa na nguvu na kasi.
Ametoa mwito kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuteua wasaidizi wa makocha wa kigeni wenye upeo wa mchezo huo. Alisema wasaidizi wanaoteuliwa sasa, wanashindwa kugundua makosa ya wachezaji na kutoa ushauri wa maana kwa makocha wa kigeni.
Tino alizaliwa mwaka 1956 katika hospitali ya Ocean Road mjini Dar es Salaam, akiwa mtoto wa tano katika familia ya watoto tisa wa mzee Peter Agustino. Familia hiyo ilikuwa ikiishi maeneo ya Msimbazi, Dar es Salaam.
Alianza kucheza soka mwaka 1967 katika timu ya mtaani ya Bonde Sports kabla ya kuhamia Young Kinya ya Kariakoo na baadaye Englebeth ya Manzese. Kutokana na kipaji alichokuwa nacho katika soka, aliajiriwa na kiwanda cha nguo cha urafiki na kuichezea kuanzia mwaka 1974 akiwa na marehemu Gibson Sembuli, Adam Juma, Awadh Gesani, Abdulrahman Juma na Wengineo.
Mwaka 1975 alihamia Mwanza na kujiunga na Mwatex, aliyoichezea kwa miezi mitatu. Mwaka huo huo, alikwenda Arusha na kujiunga na klabu ya Kurugenzi kabla ya kuhamia Tanga na kujiunga na African Sports.
Aliichezea African Sports hadi mwaka 1979 akiwa na baadhi ya wachezaji waliong'ara nchini enzi hizo kama vile Abdalla Luo, Kassim Mwabuda, Omar Bawazir, Peter Mhina, Francis Chausa na Mhando Mdeve.
Aliitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa mara ya kwanza mwaka 1977 na kuichezea hadi mwaka 1985. Aliichezea timu hiyo kwenye michuano mbalimbali ya awali ya kombe la Chalenji, Kombe la Afrika na Kombe la Dunia.
Mwaka 1980, aliihama African Sports na kujiunga na Pan African ya Dar es Salaam. Aliichezea klabu hiyo kwa miaka minne katika ligi ya Tanzania Bara na michuano ya Kombe la Washindi la Afrika kabla ya kuhamia Yanga hadi alipostaafu soka mwaka 1989.

No comments:

Post a Comment