KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, December 6, 2011

KOCHA MPYA WA SIMBA ATOA YA MOYONI



Na Ezekiel Kamwaga

KLABU ya soka ya Simba hivi karibuni ilimtangaza Profesa Milovan Cirkovic kuwa kocha wake mkuu akichukua nafasi ya Moses Basena.Cirkovic (inatamkwa Chirkovich) ameingia mkataba wa miezi sita kuifundisha Simba na mkataba huo umeanza rasmi Desemba Mosi mwaka huu.Tovuti ya Simba, www.simba.co.tz ilifanya naye mahojiano hivi karibuni ambapo alieleza kwa kirefu mambo ambayo wapenzi wa Simba na mchezo wa soka nchini kwa ujumla wangependa kuyafahamu.Pata uhondo.

Simba: Karibu tena Simba Sports Club.

Milovan: Ahsante sana. Naipenda Simba. Naipenda Tanzania na kwa kweli nimefurahi kurejea hapa.

Simba: Tanzania na Serbia ni mbali kwelikweli. Kabla hujaja Tanzania kuifundisha Simba kwa mara ya kwanza miaka ya nyuma, je ulikuwa umewahi kusikia chochote kuhusu Simba au Tanzania?

Milovan: Kusema ukweli, sikuwa nimewahi kusikia chochote kuhusu Simba hadi nilipokuja kufundisha. Kila kitu nilikipata hapa kuhusu Simba.Hata hivyo, nilikuwa nafahamu kuhusu nchi ya Tanzania. Nilisoma shuleni na sisi tunafundishwa mengi sana katika jiografia. Na usisahau kuwa mimi nimewahi kuwa mwalimu wa Chuo Kikuu na hivyo kwa wasomi ni rahisi kufahamu mambo ya nchi za mbali.

Simba: Jambo gani ambalo bado unalikumbuka kuhusu Tanzania ulipokuja mara ya kwanza.

Milovan: (Anacheka). Siku moja nilikuwa matembezini na Hagila (Evarist, miongoni mwa waliokuwa viongozi wa Simba wakati Milovan alipokuja mwaka 2007) na ghafla nyani akatokea mbele yetu.Sitaisahau siku hiyo kwa sababu hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kwangu kumwona nyani uso kwa uso. Mara zote nimekuwa nikiwaona kupitia luninga.Hilo nalikumbuka sana.

Simba: Turudi kwenye soka sasa. Hebu kwanza tueleze kwa kifupi historia yako kisoka

Milovan: Ok. Nilizaliwa katika iliyokuwa Yugoslavia ya zamani katika mji wa Cacak (inatamkwa tatak) mwaka 1955.Nilicheza soka hadi kiwango cha daraja la kwanza na niliachana na soka wakati nilipovunjika mguu mpirani wakati nilipokuwa na miaka 31. (Anaonyesha kovu la jeraha lake mguuni).Niliwahi kuchezea klabu maarufu ya Partizan Belgrade na mara baada ya kuumia nikaingia katika masuala ya taaluma kiasi cha kuwa mwalimu katika Chuo Kikuu cha Belgrade.Nina vyeti mbalimbali vya ukocha kuanzia Shahada ya Chuo Kikuu katika Elimu ya Viungo (Physical Education) na nimefundisha pia somo hilo vyuo vikuu na ndiyo maana naitwa Profesa.Nina leseni ya ukocha inayotambuliwa na UEFA, pamoja na vyeti vingine vinavyotambuliwa.

Simba: Kwanini uliamua kuwa kocha wa soka?

Milovan: Mara baada ya kuachana na kucheza soka mapema, niliona njia pekee ya kuendelea kubaki katika mchezo huu ni kuwa kocha.Napenda sana mpira wa miguu na sidhani kama ningeweza kufanya kingine chochote kwenye maisha yangu zaidi ya kucheza au kujihusisha kwa namna yoyote ile na mchezo huu.

Simba: Serbia si miongoni mwa nchi kubwa za Ulaya lakini imekuwa na sifa kubwa ya kutoa makocha wazuri duniani hususani katika nchi za Afrika na Asia. Nini unafikiri ni siri ya mafanikio haya?

Milovan: Kwanza tunapenda sana mpira –sisi raia wa Serbia. Kwa hiyo kuwa kocha au mchezaji mzuri kunakuja tu kwenye damu.Lakini la pili ni kuwa kuna vyuo vingi sana vya ukocha kule kwetu na pia tuna uwezo wa kuishi katika mazingira magumu.Mimi nimekuja Tanzania na sina ndugu, jamaa wala rafiki yeyote. Kila kitu nawaamini ninyi. Inahitaji roho ngumu kidogo kuchukua maamuzi magumu kama haya.Hizo zinaweza kuwa sababu za msingi zaidi.

Simba: Nimesikia kuwa mmoja wa marafiki zako wa karibu zaidi ni Milovan Rajevac, Kocha aliyeipeleka Ghana katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika. Je taarifa hizi zina ukweli wowote?

Milovan: Milovan ni rafiki yangu. Nilipokuwa kocha wa FC Borak Cacak mwaka 2008, yeye alikuwa msaidizi wangu kwa maana ya kocha msaidizi.Ni rafiki yangu wa karibu sana.

Simba: Nini falsafa yako ya soka? Unataka soka ichezweje na wachezaji wako?

Milovan: Rahisi. Timu zote zinazofundishwa na mimi zinakuwa na sifa ya kucheza soka la pasi nyingi na zinazomiliki mpira.Nataka timu ianze kucheza kuanzia nyuma. Nafahamu kuwa kuna wakati timu inaweza kutengeneza nafasi na kufunga kwa pasi chache lakini si kitu cha kutokea mara kwa mara.Nataka timu icheze kama Barcelona ya Hispania. Mimi nimeanza kuipenda Barcelona zamani kabla hata Josep Guardiola hajawa kocha wa timu hiyo.Siku zote Barcelona imekuwa ikicheza vizuri. Real Madrid inatwaa makombe lakini Barca inacheza soka la kuvutia zaidi. Soka ni burudani na inanoga zaidi kama inaendana na ushindi. Hata Arsenal ya miaka mitano iliyopita ilikuwa inacheza soka ninayoipenda.Ninachokisema ni hivi, Simba si Barcelona. Lakini inaweza kucheza kama Barca kwa kiwango chake. Huo ndiyo mtazamo wangu.

Simba: Kuna wachezaji wowote wa Simba uliowafundisha miaka minne iliyopita na bado unawakumbuka?

Milovan: Namkumbuka Chollo (Nassor Said Masoud), mimi ndiye niliyembadilisha kucheza kutoka kiungo na kuwa mlinzi wa pembeni.Nilimuona tu namna ya uchezaji wake na nikashauriana na wenzangu katika benchi la ufundi kuwa anafaa kuwa mlinzi wa pembeni.Nimefurahi kuwa sasa ni mlinzi wa kulia tegemeo kwa taifa. Namkumbuka pia Juma Nyoso, Victor Costa, ingawa alikuwa anaumwa goti wakati nilipokuja na Emmanuel Gabriel ambaye alikuwa anajua sana kufunga.
Nimeangalia michuano ya Chalenji na tayari nimewaona Jabu, Kapombe, Kaseja, Kazimoto na Okwi. Wote ni wachezaji wazuri na nasubiri kwa hamu kufanya nao kazi.

Simba: Kikosi cha pili cha Simba maarufu kwa jina la U20, hivi karibuni kimetwaa Kombe la Uhai na wengi wanakizatama kama sehemu muhimu ya mafanikio ya Simba katika miaka ijayo. Una mpango gani na kikosi hiki.

Milovan: Kwanza nimefurahi sana kwa Simba kuwa na kikosi hiki cha vijana. Huu ndiyo utaratibu duniani kote, huwezi kuwa na timu nzuri ya wakubwa kama huna timu nzuri ya vijana.Kwa bahati nzuri, mimi nina historia ya kufundisha timu za wakubwa na watoto ndani na nje ya Serbia. Nina uzoefu na najua nini wanahitaji.Sifa yangu moja kubwa ni kuwa, kama kijana akiwa na uwezo, hata kama ni mdogo, mimi ninampa nafasi. Lakini ni lazima nihakikishe yuko tayari kiakili kukabiliana na changamoto alizonazo.Kama mchezaji ni mzuri, atapata nafasi.

Simba: Hebu tueleze kuhusu familia yako kwa ufupi.

Milovan: Nina mke, Dionezia na watoto watatu wa kike – Anna, Sara na Marta.S: Unavuta sigara gani? Ngapi kwa siku.M: Navuta Malboro. Kwa kawaida huwa navuta pakiti moja na nusu kwa siku.

Simba: Una jina lolote la utani?

Milovan: Ukienda Serbia na ukaniulizia kwa jina la Milovan hutonipata. Uliza Profesa Cirko (Profesa Chirco). Kwa hiyo, sina tatizo kama Watanzania watakuwa wakiita kwa ufupi Chirco.

Simba: Miongoni mwa wanasoka maarufu zaidi kutoka Serbia kwa sasa ni Nemanja Vidic. Je, unamfahamu kivipi?

Milovan: Sifahamiani naye kibinafsi. Isipokuwa anatoka katika eneo la Uzice (tamka Ujitse), kijiji kinachofuata kutoka cha kwangu cha Cacak.

Simba: Unawaahidi nini wapenzi na wanachama wa Simba watakaosoma mahojiano haya.

Milovan: Nawaomba waipe timu muda wa kunielewa na mimi kuwaelewa wachezaji wangu. Soka si sawa na spea ya gari ambayo ukiiweka gari inawaka hapohapo.Itachukua muda kidogo kuelewana na hivyo naomba uvumilivu kutoka kwa washabiki. Kwa bahati nzuri washabiki wa Simba ni watu waelewa sana na nadhani watavuta subira kidogo.
Simba: Kila la kheri kocha.

Milovan: Ahsante sana.

No comments:

Post a Comment