KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, December 6, 2011

VENGU APATA AHUENI






HALI ya msanii Joseph Shamba 'Vengu' wa kundi la Orijino Komedi inaendelea vizuri na amehamishwa kutoka kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na kulazwa kwenye wodi ya Mwaisela katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Vengu, ambaye aliwekwa kwenye chumba hicho kwa zaidi ya miezi miwili kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa, ambao bado haujawekwa wazi, alihamishiwa kwenye wodi ya Mwaisela juzi.
Akizungumza baada ya kumtembelea msanii huyo kwenye wodi hiyo juzi ili kujua maendeleo ya afya yake, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara alisema hali ya Vengu inaendelea vizuri.
Dk. Fenella alikanusha taarifa zilizosambazwa kwenye baadhi ya mitandao ya habari mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba Vengu amefariki dunia.
"Binafsi nimemtembelea wodini leo hii (juzi) na kusema kweli hali yake inaendelea vizuri kwa sababu unapotolewa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi na kuhamishiwa wodini, maana yake ni kwamba madaktari wameridhishwa na maendeleo yako,"alisema.
Dk. Fenella alisema kinachofanyika kwa sasa ni msanii huyo kuendelea kutumia dawa alizoandikiwa na madaktari huku akiendelea kufanyiwa uchunguzi zaidi wa afya yake.
Kaka wa msanii huyo,Steven Shamba alisema wanamshukuru Mungu kuona hali ya msanii huyo inaendelea vizuri baada ya kutolewa ICU.
"Tunachoshukuru ni kwamba matibabu yake yanasimamiwa na profesa na kitendo cha kutolewa chumba cha wagonjwa mahututi na kulazwa wodini kinaashiria kwamba maendeleo yake ni mazuri,"alisema.
Kiongozi wa kundi la Orijino Komedi, Sekione David, maarufu kwa jina la Seki alisema, matibabu ya Vengu kwa sasa yanagharamiwa na Rais Jakaya Kikwete hivyo kama kuna umuhimu kwa msanii huyo kupelekwa nje kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi, ndiye pekee mwenye uamuzi huo.
"Watu wengi wamekuwa wakitulalamikia kwamba kwa nini asipelekwe India kupatiwa matibabu. Tunachoweza kusema ni kwamba yanaweza kupatikana hapa hapa, kwa nini apelekwe India? Tunachoshukuru Mungu ni kwamba, matibabu yake yanagharamiwa na Rais Jakaya Kikwete,"alisema.
Seki alieleza kusikitishwa kwake na taarifa potofu zilizosambazwe kwenye mitandao wiki iliyopita, zikidai kwamba msanii huyo amefariki dunia. Alisema taarifa za aina hiyo si nzuri kwa jamii na ni vyema wahusika wapate taarifa sahihi kutoka kwa vyanzo husika vya habari kuliko kukurupuka na kueneza uvumi wa uongo.
Vengu hajaonekana kwenye vipindi vya Orijino Komedi vinavyoonyeshwa na kituo cha televisheni cha TBC 1 kwa takriban miezi miwili sasa kufuatia kulazwa Muhimbili.
Hata hivyo, bado haijawekwa wazi kuhusu ugonjwa unaomsumbua, lakini kuna habari kuwa, anasumbuliwa na maumivu ya kichwa.
Msanii huyo alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na kuweza kumwigiza Mwenyekiti wa chama cha TLP, Augustine Mrema kwa mavazi na sauti yake wakati wa maonyesho ya Orijino Komedi.

No comments:

Post a Comment