KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, December 9, 2011

Taifa Stars, Simba, Yanga hazijawakuna Watanzania

KIKOSI cha Taifa Stars

KIKOSI cha Simba


KIKOSI cha Yanga


TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars haina rekodi kubwa ya kujivunia katika michuano ya Afrika. Rekodi pekee ilizoweza kufikia ni kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1980 na fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CAN) mwaka 2010.
Mshambuliaji Peter Tino ndiye aliyeiwezesha Taifa Stars kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka 1980 baada ya kuifungia bao la kusawazisha katika mechi ya marudiano dhidi ya Zambia.
Katika mechi ya awali kati ya timu hizo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Taifa Stars iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji Thuweni Ally.
Katika mechi ya marudiano iliyochezwa mjini Ndola, Zambia ilikuwa mbele kwa bao 1-0 hadi Tino alipoifungia Taifa Stars bao la kusawazisha na hivyo kuiwezesha kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1.
Hata hivyo, Taifa Stars haikuweza kufanya vizuri katika fainali za michuano hiyo zilizochezwa mjini Lagos, Nigeria baada ya kufungwa mechi mbili na kuambulia sare mechi moja.
Katika mechi yake ya kwanza, Taifa Stars ilikubali kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Nigeria. Mabao ya Nigeria yalifungwa na Lawal, Onyedika na Odegbami wakati bao la kujifariji la Taifa Stars lilifungwa na Thuweni.
Taifa Stars ilikubali tena kipigo katika mechi yake ya pili dhidi ya Misri, ambapo ilichapwa mabao 2-1. Mabao ya Misri yalifungwa na Hassan Shehata na Mosaad Nour wakati bao la Stars lilifungwa na Thuweni.
Katika mechi yake ya mwisho, Taifa Stars iliilazimisha Ivory Coast kutoka nayo sare ya bao 1-1. Bao la Ivory Coast lilifungwa na Kobenan wakati lile la Stars lilifungwa na Thuweni.
Kufuatia matokeo hayo, Taifa Stars ilimaliza mechi za kundi lake ikiwa ya mwisho baada ya kuambilia pointi moja wakati Nigeria ilishika usukani kwa kuwa na pointi tano.
Hatua nyingine ya juu iliyofikiwa na Taifa Stars katika michuano ya kimataifa ni kufuzu kucheza fainali za CAN mwaka 2009 nchini Ivory Coast baada ya kuitoa Sudan.
Katika mechi yake ya kwanza, Taifa Stars ilipigwa mweleka wa bao 1-0 na Senegal kabla ya kuibuka na ushindi wa idadi hiyo ya bao dhidi ya Ivory Coast.
Hata hivyo, matumaini ya Stars kusonga mbele yalizimwa na Zambia baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1. Zambia ndiyo iliyoongoza kundi hilo na kufuzu kucheza nusu fainali.
Rekodi nyingine ya kujivunia kwa Taifa Stars ni kufuzu kucheza hatua ya nusu fainali katika michezo ya All Africa Games iliyofanyika mwaka 1973 mjini Lagos, Nigeria.
Katika michuano hiyo iliyochezwa kwa mtindo wa ligi, Taifa Stars ilitoka sare mechi mbili dhidi ya Nigeria na Misri na kufungwa mechi ya mwisho mabao 2-1 na Algeria.
Kabla ya hatua hiyo, Taifa Stars ilitoka suluhu na Nigeria A, ikaichapa Nigeria B mabao 2-1 kabla ya kutoa kipigo cha bao 1-0 kwa Ghana na Togo. Mshambuliaji Maulid Dilunga ndiye aliyeibeba Taifa Stars baada ya kuifungia mabao yote kwenye michuano hiyo.
Taifa Stars haijawahi kufika hatua za mbali katika michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia. Mara zote ilizoshiriki, imekuwa ikitolewa aidha raundi ya kwanza ama ya pili.
Katika michuano ya Kombe la Chalenji, Tanzania Bara ililitwaa kombe hilo kwa mara ya kwanza mwaka 1974 kabla ya kusubiri kwa miaka 20 na kulitwaa tena mwaka 1994. Bara ilitwaa kombe hilo kwa mara ya mwisho mwaka 2010 baada ya kuifunga Ivory Coast bao 1-0 kwa njia ya penalti katika mechi ya fainali.
Kwa upande wa timu za taifa za vijana, hatua pekee ya juu ilifikiwa na timu ya vijana wa chini ya miaka 17, Serengeti Boys mwaka 2004, ilipofuzu kucheza fainali za Afrika baada ya kuitoa Zimbabwe.
Hata hivyo, Shirikisho la Soka Afrika (CAF), liliiengua Serengeti Boys kushiriki kwenye fainali hizo zilizofanyika Gambia baada ya kubainika kuwa, ilimchezesha mchezaji Nurdin Bakari, ambaye umri wake ulikuwa zaidi ya miaka 17.
Mbali na Serengeti Boys kuenguliwa kwenye fainali hizo, CAF pia iliifungia Tanzania kushiriki kwenye michuano inayozingatia umri kwa kipindi cha miaka miwili kwa kosa hilo.
Timu ya vijana wa chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes haijawahi kufika mbali katika michuano yote iliyoshiriki kama ilivyokuwa kwa timu ya vijana wa chini ya miaka 23, Vijana Stars. Timu hizo zimekuwa zikitolewa hatua ya awali kila ziliposhiriki michuano ya Afrika na ile ya Olimpiki.
Timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars iliyoanzishwa mwanzoni mwa miaka ya 2000, imekuwa ikijitutumia katika michuano ya Afrika na kufuzu kucheza fainali mara mbili.
Mara ya kwanza ilikuwa mwaka juzi ilipofuzu kucheza fainali hizo nchini Afrika Kusini kabla ya kufuzu kucheza fainali za All African Games zilizofanyika mwaka huu nchini Msumbiji.
Katika fainali za mwaka juzi, Twiga Stars ilishindwa kufanya vizuri kutokana na wachezaji wake kutokuwa na uzoefu wa kutosha katika michuano ya kimataifa.
Akina dada hao walipoteza mechi zote tatu za hatua ya makundi, ambapo katika mechi ya kwanza, walichapwa mabao 2-1 na wenyeji Afrika Kusini. Katika mechi yake ya pili, Twiga Stars ilichapwa mabao 3-2 na Mali kabla ya kucharazwa mabao 3-0 na Nigeria.
Twiga Stars pia ilichemsha katika fainali za mwaka huu za All Africa Games zilizofanyika mjini Maputo, Msumbiji. Katika mechi yake ya kwanza, ilitoka sare ya mabao 2-2 na Afrika Kusini, ikachapwa mabao 2-1 na Ghana kabla ya kufungwa idadi hiyo ya mabao Zimbabwe.

Simba ndiyo timu pekee iliyoweka rekodi ya juu katika michuano ya kimataifa, ambapo mwaka 1993 ilifuzu kucheza fainali ya Kombe la CAF, lakini ikafungwa na Stella Abidjan ya Ivory Coast.
Katika mechi ya awali ya fainali iliyochezwa mjini Abidjan, timu hizo mbili zilishindwa kutambiana baada ya kutoka suluhu. Simba ilicheza fainali hiyo ikiwa chini ya makocha Abdalla Kibadeni na Eshente kutoka Ethiopia.
Matokeo hayo yaliwapa imani kubwa mashabiki wa soka nchini kwamba, huenda Simba ingeweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutwaa taji la Afrika.
Maandalizi kabambe ya kusherehekea ushindi yalifanyika. Kamati maalumu zikaundwa kwa ajili ya kuhakikisha ushindi unapatikana nyumbani na kanga zikachapishwa zikiwa na maandishi ‘Simba Bingwa CAF 1993’.
Hata hivyo, mambo yaligeuka katika mechi ya marudiano iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Katika mechi hiyo, iliyoweka rekodi ya kuhudhuriwa na mashabiki lukuki, Simba ilichezea kichapo cha mabao 2-0.
Kipigo hicho kilizusha huzuni kubwa, si kwa wachezaji tu wa Simba, bali hata kwa viongozi, wanachama na mashabiki wa klabu hiyo, ambao walishuhudia Rais Ali Hassan Mwinyi akikabidhi kombe la ubingwa kwa nahodha wa Stella Abidjan.
Kabla ya kufuzu kucheza fainali hiyo, Simba ilikuwa imeweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika mwaka 1974 huku ikitoa vichapo kwa vigogo kadhaa vya soka. Ilicheza hatua hiyo ikiwa chini ya Kocha Nabi Camara kutoka Guinea.
Katika mechi ya awali ya nusu fainali iliyochezwa mjini Dar es Salaam, Simba iliichapa Mehala El-Kubra ya Misri bao 1-0, lakini ikatolewa kwa njia ya penalti baada ya Wamisri kushinda mechi ya marudiano kwa idadi hiyo ya bao.
Simba pia iliweka rekodi ya kufuzu kucheza ligi ya mabingwa wa Afrika hatua ya makundi mwaka 2003, ikiwa chini ya Kocha James Siang'a kutoka Kenya, baada ya kuwatoa waliokuwa mabingwa watetezi, Zamalek ya Misri kwa njia ya penalti, kufuatia matokeo ya jumla kuwa sare ya bao 1-1.
Katika hatua hiyo ya makundi, Simba ilishinda mechi mbili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, dhidi ya Enyimba na ASEC, lakini ikakubali vipigo vitatu ugenini. Ilimaliza hatua hiyo ikiwa ya pili kutoka mkiani.
Rekodi zingine za kujivunia kwa Simba ni kuweza kuziadhiri timu vigogo za Misri katika mechi tofauti za michuano ya kimataifa. Mwaka 1974 iliichapa mehara El-Kubra bao 1-0 mjini Dar es Salaam, miaka tisa baadaye iliicharaza Al-Ahly mabao 2-1 mjini Mwanza, mwaka 1995 iliinyuka Arab Contractors mabao 3-1 kabla ya kuilaza Ismailia bao 1-0 mjini Dar es Salaam.
Pengine rekodi pekee ya kujivunia kwa Simba ni kutwaa ubingwa wa michuano ya klabu za Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame) miaka ya 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002. Ndio timu pekee iliyotwaa kombe hilo mara nyingi, ikilinganishwa na klabu zingine za ukanda huu.
YANGAYanga ni timu nyingine ya Tanzania iliyoweka rekodi ya kufuzu kucheza robo fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika mara mbili mwaka 1969 na 1970, lakini mara zote ilitolewa na Asante Kotoko ya Ghana.
Katika robo fainali ya mwaka 1969, Yanga ilitolewa na Asante Kotoko kwa njia ya kura ya shilingi baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya bao 1-1.
Katika robo fainali ya pili mwaka 1970, Yanga ilikutana tena na Asante Kotoko, ambapo katika mechi ya awali, zilitoka sare ya bao 1-1 na katika mechi ya marudiano, hazikufungana.
Mshindi wa pambano hilo ilibidi apatikane katika muda wa nyongeza, lakini kutokana na giza kutanda uwanjani, mechi ilivunjika dakika ya 19 na hivyo kuhamishiwa kwenye uwanja huru wa mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Katika mechi hiyo ya tatu, Yanga ilikubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Asante Kotoko na kutolewa kwenye hatua hiyo. Kikosi cha Yanga wakati huo kilikuwa chini ya Victor Stanculescu kutoka Romania.
Yanga pia iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kufuzu kucheza ligi ya mabingwa wa Afrika mwaka 1998, ikiwa chini ya kocha Raoul Shungu kutoka Congo, lakini ilivurunda kwenye hatua ya makundi. Ligi hiyo ilianzishwa rasmi mwaka 1997.
Timu hiyo kongwe nchini ilimaliza mechi za makundi ikiwa mkiani baada ya kupokea kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa ASEC ya Ivory Coast katika mechi yake ya mwisho iliyochezwa mjini Dar es Salaam.
Katika hatua hiyo ya makundi, Yanga pia ilipokea kipigo kizito cha mabao 6-0 kutoka kwa Raja Casablanca ya Morocco na kutoka sare ya bao 1-1 na Manning Rangers ya Afrika Kusini.
Rekodi pekee ya kujivunia kwa Yanga ni ile ya kutwaa ubingwa wa klabu za Afrika Mashariki na Kati mara nne, mwaka 1975, 1993, 1999 na 2010.
Klabu zingine za Tanzania zilizowahi kushiriki michuano ya Afrika ni Cosmopolitan (1967), Mseto (1975), Pan African (1982), Tukuyu Stars (1986), Coastal Union (1988), Mtibwa Sugar (1999 na 2000), lakini zote ziliishia hatua ya awali.

No comments:

Post a Comment