KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, March 20, 2016

TWIGA STARS KULIPA KISASI KWA WAZIMBABWE LEO?


Timu ya soka ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars inatarajiwa kuwakabili wenyeji wao Zimbabwe (Mighty Warriors) katika mchezo wa marudiano wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AWC) utakaofanyika leo kwenye Uwanja wa Rufalo jijini Harare.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Machi 4 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam, Twiga Stars ililala mabao 2-1 dhidi ya wapinzani wao hao na leo inahitaji ushindi wa kuanzia 2-0 ili iweze kusonga mbele.
Kocha mkuu wa Twiga Stars, Nasra Juma, alisema kwamba kikosi chake kiko tayari kwa mapambano na wanataka kurudia mafanikio waliyopata 2010 kwa kushiriki fainali hizo zilizofanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Nasra alisema kuwa sasa wanaingia mchezo wakiwa wanawafahamu wapinzani wao tofauti na ilivyokuwa katika mechi ya kwanza ambayo walikubali kichapo.
"Tunajua aina ya wachezaji na mfumo wanaocheza, tumejipanga kufanya vizuri kwa sababu nia, sababu na uwezo wa kuwaondoa Zimbabwe wakiwa kwao tunao," alisema Nasra.
Mkuu wa msafara wa timu hiyo na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Amina Karuma, aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu kwamba wachezaji wote wako katika hali nzuri na wanasubiri muda wa mchezo ufike.

No comments:

Post a Comment