KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 9, 2012

SHARO MILIONEA: STAILI YANGU YA USHAROBARO NI YA PEKEE



MSANII nyota wa vichekesho na muziki wa kizazi kipya nchini, Hussein Mkiety amesema amebuni staili ya usharobaro kwa lengo la kujitofautisha na wasanii wengine.
Hussein, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Sharo Milionea, alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, ubunifu wake huo umemwezesha kupata mashabiki wengi katika fani zote mbili.
Alisema licha ya kuwepo kwa tabia ya watu wanaojikweza kwa muda mrefu, wakiwa maarufu kwa jina la ‘mabradha meni’, staili analiyoibuni ya watu wa aina hiyo imekuwa na mvuto zaidi.
Alivitaja vitu vingine alivyovibuni kwa lengo la kuupa mvuto ‘ubradha meni’ kuwa ni pamoja na uongeaji wake kwa kupinda mdomo, uvaaji, utembeaji, unyoaji nywele na kubandika plasta usoni.
“Staili ya mabradha meni asili yake hasa ni Wamarekani. Kila wakisema neno, lazima wamalizie kwa kusema ‘you know man’. Nami nimeiiga, lakini nimeongezea vionjo vingine zaidi,”alisema.
Hussein alisema alianza kujihusisha na uigizaji tangu akiwa shule ya sekondari na kwamba amewahi kucheza filamu moja na baadhi ya wasanii maarufu kama vile Masanja Mkandamizaji na McReagan wa kundi la Orijino Komedi.
Aliongeza kuwa, fani ya uchekeshaji ni asili yake tangu akiwa mdogo kutokana na kuwafurahisha vijana wenzake kila walipokuwa wakikutana kwa mazungumzo vijiweni kwa kubuni maneno yenye mvuto.
“Kila nilipokuwa nikikaa na kuzungumza na wenzangu, niliposema maneno fulani, walikuwa wakivutiwa nayo sana na kuniona mtu wa ajabu, yaani mchekeshaji,”alisema.
Hussein alisema aliamua kujitosa kwenye fani ya muziki baada ya kujibaini kwamba, anacho kipaji cha fani hiyo na hadi sasa amesharekodi nyimbo nne.
Alizitaja nyimbo hizo kuwa ni Tusigombane, Chuki bure aliomshirikisha Dully Sykes, Nawazamisha aliomshirikisha Nukta na Hawataki alioimba kwa kushirikiana na Kanali Top na Richard Mavoko.
Kwa mujibu wa Hussein, aliweza kurekodi nyimbo hizo kwa msaada mkubwa wa promota maarufu wa muziki nchini, Ustaadh Juma Namusoma, ambaye kwa sasa anamiliki kundi la Watanashati.
Hussein alisema kwa sasa ameshampata mdhamini, atakayekuwa akigharamia kurekodi nyimbo zake pamoja na kurekodi kanda za video, lakini hakuwa tayari kumtaja.
Alisema kwa kumtumia mdhamini huyo, ameanza kuandaa nyimbo zake mpya, ambazo atazirekodi kwa kushirikiana na msanii mwenzake nyota wa vichekesho, anayejulikana zaidi kwa jina la Kitale.
Alikiri kuwa, licha ya kurekodi nyimbo nne hadi sasa, bado hajaweza kupata mafanikio makubwa kimuziki kutokana na fani hiyo kukumbwa na vikwazo vingi.
Alisema mafanikio pekee aliyoyapata ni kujulikana na mashabiki wengi wa muziki na pia kupata marafiki wapya kila kukicha.
“Kwa sasa nitaendelea kurekodi wimbo mmoja mmoja hadi hapo mambo yatakapokuwa mazuri ndipo nitakaporekodi albamu,”alisema msanii huyo.
Alipoulizwa madai kuwa, amekuwa akipenda kujifagilia katika vichekesho anavyocheza pamoja na nyimbo zake, Hussein alisema huo ni uigizaji, lakini sivyo alivyo.
Hussein alikiri kuwa, miongoni mwa watu waliomwonyesha njia katika fani ya uigizaji ni msanii Kiwewe wa kundi la Ze Comedy. Lakini alikanusha madai kwamba, amewahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mcheza filamu, Shilole.
“Shilole ni rafiki yangu na ni kama dada yangu. Vivyo hivyo kwa Mzee Majuto, namuheshimu nampenda na kumuheshimu kama baba yangu, ‘alisema.
Msanii huyo pia alikanusha madai kuwa, aliwahi kugombania jina la Sharobaro na msanii Bob Junior. Alisema jina la kiusanii analotumia ni Sharo Milionea na siyo Sharobaro.
Hussein amekiri kuwa, katika wimbo wa Ferouz wa Starehe gharama, alikubali kuvua nguo zake kwenye picha ya video baada ya kulipwa kitita cha sh. milioni moja na nusu, ambacho alikielezea kuwa kwake ni kikubwa.

No comments:

Post a Comment