KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, August 28, 2012

KESI YA LULU YAENDELEA KUPIGWA KALENDA

KESI ya tuhuma za mauaji inayomkabili msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael au ‘Lulu’ imeendelea kupigwa kalenda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Msanii huyo anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba, alipandishwa kizimbani jana mahakamani hapo, kesi hiyo ilipotajwa.
Wakili wa Serikali Leonard Chalo alidai mbele ya Hakimu Mkazi Augustino Mbando, kuwa shauri hilo limekuja kwa kutajwa.
Hata hivyo, Hakimu huyo alisema jalada la kesi hiyo lipo mahakama ya juu ambapo alitaka kujua hatua iliyofikiwa kuhusu suala la mshitakiwa huyo kutotakiwa kupandishwa kizimbani mahakamani hapo.
Wakili wa utetezi Peter Kibatala alidai ameshawasiliana na Hakimu Mkazi Mfawidhi Ilvin Mugeta ambaye alimweleza kwamba ataandika barua kwenda Mahakama Kuu kuelezea sababu za Lulu kufikishwa Kisutu.
Hakimu huyo aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 10, mwaka huu kwa kutajwa.
Baada ya Lulu kupandishwa kizimbani Mahakama ya Kisutu, mawakili wake waliwasilisha maombi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, kuomba kufanya uchunguzi wa umri wa mshitakiwa huyo.
Jaji Dk. Fauz Twaib aliyepangiwa kusikiliza maombi hayo alikubali mahakama hiyo kufanyia uchunguzi umri wa Lulu na kuamuru mshitakiwa huyo kutopelekwa Kisutu bali awe anafikishwa Mahakamani hapo.

No comments:

Post a Comment