MWENYEKITI wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Dioniz Malinzi, amezindua rasmi michezo ya nne ya mbio za Rock City Marathon, zitakazofanyika kuanzia Oktoba 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika mjini Dar es Salaam jana, Malinzi alisema huu ni wakati wa kukufua vipaji vya mchezo wa riadha nchini.
“Kwanza nawashukuru Kampuni ya Capital Plus Internationa kwa kuendelea kuandaa mbio hizi kwa miaka mine sasa. Sio siri michezo Tanzania imedorora, kwani tumechukua dhamana ya michezo, lakini baadhi ya watu wamekuwa walafi, wanajenga majumba Mbezi Beach na kuendesha magari ya kifahari.
“Hii yote imechangiwa na dhamana ya uongozi wa michezo kuwapa walafi ambao wametufikisha hapa. Nawaomba Capital Plus International msiishie hapa, tunataka sasa tufufue vipaji vya riadha na mwaka huu tumeamua tuwe na mashindano ya taifa ya riadha,” alisema Malinzi.
Mashindano hayo yamevutia wadau wengi waliojitokeza kudhamini mbio hizo, ambao ni Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), African Barrick Gold, Nyanza Bottlers, Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF), Geita Gold Mine, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Sahara Communications, Shirika la Ndege Tanzania (ATC), New Mwanza Hotel, Airtel na New Africa Hotel.
Mbio za mwaka huu zitahusisha mashindano mbali mbali kama vile mbio za nyika za kilomita tano (ambazo sio za ushindani) , mbio za nusu marathon za kilomita 21 na mbio za kujifurahisha maarufu kama 'fun race'.
Mbio zingine ni za walemavu za kilomita tatu, mbio za watu wazima za kilomita tatu na mbio za watoto kuanzia miaka saba hadi 10 zenye urefu wa kilomita mbili.
Msemaji wa Capital Plus International, Dk. Ellen Otaru, alisema mbio hizo zinakwenda sambamba na kuhamasisha utalii wa ndani kupitia sekta ya michezo, ambapo washiriki watatoka Ziwa Victoria na nchi jirani za Kenya, Uganda, Afrika Kusini na baadhi ya mataifa ya Ulaya.
“Ningependa kutoa shukrani kwa wafadhili mbali mbali waliofanikisha mashindano haya, nasi Capital Plus International tunataka kuwahakikishia kuwa tunakuza riadha nchini na kuleta medali za dhahabu,” alisema.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Riadha Tanzania (RT), William Kalage, alisema wameridhia uwezo wa Capital Plus International kuandaa mbio hizo kwa mara ya nne kwa ufanisi.
“Sote tunatambua mchezo wa riadha ndio ulioipa sifa nchi yetu, lakini kwa sasa umedorora. Safari ya kuiletea medali nchi yetu imeanza na lazima tuwekeze kwenye riadha ili tupate medali,” alisema Kalage
No comments:
Post a Comment