KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, August 27, 2012

ATONG, MREMBO WA SUDAN KUSINI ALIYETWAA TAJI LA MREMBO WA AFRIKA

MREMBO Atong Demach wa Sudan Kusini mwishoni mwa wiki iliyopita aliushangaza ulimwengu baada ya kutawazwa kuwa mrembo wa Afrika katika shindano la dunia lililofanyika katika mji wa Ordos uliopo kaskazini mashariki mwa China.
Atong alitwaa taji hilo ikiwa ni mara ya kwanza kwa Sudan Kusini kushiriki katika shindano hilo baada ya kujitenga na Sudan mwaka jana na kuwa nchi huru.
Katika shindano hilo lililowashirikisha warembo zaidi ya 100 kutoka katika nchi mbali mbali duniani, Wenxia Yu wa China alitawazwa kuwa mrembo mpya wa dunia 2012.
Wenxia alivishwa taji hilo na mrembo wa dunia wa mwaka 2011, Ivian Sarcos wa Venezuela. Lilikuwa taji la 62 tangu mashindano hayo yalipoanzishwa mwaka 1951.
Akiwa anaiwakilisha nchi yake kwa mara ya kwanza, Atong aliwashangaza mashabiki wa fani ya urembo duniani kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha katika mashindano ya hatua za awali.
Mbali na kutwaa taji la Afrika, mrembo huyo, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 24 pia alitwaa taji la mwanamitindo bora, ambalo ni miongoni mwa mataji madogo yanayoshindaniwa katika shindano hilo.
Atong aliteka hisia za watamazaji wakati wa shindano la mwanamitindo bora lililofanyika kwenye uwanja wa Dongsheng, ambapo alipendeza mno kwa mavazi, miondoko yake, mwonekano wake na pozi zake za picha.
Atong alikuwa miongoni mwa warembo 15 waliotinga hatua ya nusu fainali, akiwa na washiriki wenzake kutoka katika nchi za Kenya, Indonesia, Netherlands, USA, Philippines, Spain, Brazil, England, Wales, China, Jamaica, Australia, Mexico na India. Baadaye alitinga hatua ya fainali, akiwa na washiriki wenzake saba.
Mbali na Atong, warembo wengine waliotinga nusu fainali ya shindano hilo walitoka nchi za Jamaica, India, Australia, Brazil, China PR na Wales.
Kutinga hatua ya fainali kwa mrembo huyo ndiko kulikovuta hisia za watazamaji wengi wa shindano hilo, ambao walianza kufuatilia nchi anayoiwakilisha.
Sudan Kusini imeungana na nchi zingine kadhaa kutwaa taji la mrembo wa Afrika katika shindano hilo, ambapo Afrika Kusini inaongoza kwa kulitwaa mara 11.
Mwaka jana, taji hilo lilinyakuliwa na Bokang Montjane wa Afrika Kusini, ambapo pia alitinga fainali ya shindano la dunia. Mwaka 2010, taji hilo lilinyakuliwa na Emma Wareus wa Botswana.
Atong ni mwanafunzi wa mwaka wa mwisho katika Chuo Kikuu cha Juba, kilichopo mjini Juba. Moja ya malengo yake ya baadaye ni kuwasaidia watu wenye matatizo, hasa watoto na pia kuwa mtetezi wa uhifadhi wa mazingira.
Binti huyo kutoka mji wa Bor uliopo kando kando ya Mto Nile alisema kabla ya shindano hilo: “Naona fahari kuiwakilisha nchi yangu kwa mara ya kwanza katika shindano la dunia na najivunia urembo wenye malengo.”
Sudan Kusini inakadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni nane. Uamuzi wake wa kujitenga na Sudan ulitokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka kadhaa na kusababisha vifo vya maelfu ya watu wasiokuwa na hatia.
Ushindi wa taji la urembo la Afrika uliotwaliwa na Atong ni miongoni mwa mafanikio kadhaa, ambayo nchi hiyo inayatarajia katika miaka michache ijayo.
Shindano la kumsaka mrembo wa dunia liliasisiwa na Eric Morley mwaka 1951, likiwashirikisha wasichana 26 wa Uingereza.
Kwa sasa, shindano hilo linaendeshwa na Julia Morley, mke wa Eric, ambaye alifariki dunia mwaka 2000. Nchi 130 hushiriki katika shindano hilo kila mwaka.
Mwaka 2001, mrembo wa Nigeria, Agbani Darego alifanikiwa kutwaa taji la mrembo wa dunia na mwaka uliofuata, shindano hilo lilifanyika katika mji wa Abuja nchini humo.

No comments:

Post a Comment