UJIO wa beki wa kimataifa wa Rwanda, Mbuyu Twite umeendelea kuwa kitendawili baada ya kushindwa kuwasili nchini jana kujiunga na Yanga.
Badala yake, uongozi wa klabu ya Yanga umesema beki huyo wa zamani wa APR ya Rwanda sasa anatarajiwa kutua nchini leo saa tisa alasiri.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, taratibu zote za kumwezesha Twite kuja nchini leo zimekamilika.
Awali, Twite ilikuwa awasili na kikosi cha Yanga mwanzoni mwa wiki hii, lakini alishindwa kufanya hivyo kwa madai kuwa, alikwenda kwao Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuchukua familia yake.
Baadaye kulikuwepo na taarifa kwamba beki huyo angetua juzi au jana, lakini mara zote ameshindwa kufanya hivyo na kumweka kwenye wakati mgumu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Tom Saintfiet.
“Twite atatua nchini kesho (leo). Alibaki Rwanda kwa sababu za msingi, nawaomba mashabiki wa Yanga wajitokeze kwa wingi kwenda kumpokea kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam,”alisema.
Sendeu aliponda tishio lililotolewa na viongozi wa klabu ya Simba kwamba, watahakikisha wanamkamata mchezaji huyo mara atakapotua nchini kwa tuhuma za kuwatapeli.
“Hao wanaodai kwamba wana RB ya kumkamata Twite kutoka polisi Interpool wanajisumbua kwa sababu wanachokifanya ni kichekesho,”alisema Sendeu.
Ofisa Habari huyo wa Yanga alisema Twite anatarajiwa kujiunga moja kwa moja na Yanga kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, inayotarajiwa kuanza Septemba 15 mwaka huu.
Yanga imekuwa ikifanya mazoezi yake kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola, Dar es Salaam na inatarajiwa kucheza mechi nyingine ya kirafiki Jumamosi kwa kumenyana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa.
Kwa mujibu wa Sendeu, iwapo mambo yatakwenda vizuri, Twite huenda akashuka dimbani kucheza mechi hiyo na kutambulishwa rasmi kwa mashabiki wa Yanga.
Katika hatua nyingine, habari kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, kuchelewa kuwasili nchini kwa mchezaji Mbuyu Twite kumemkera Kocha Tom Saintfiet.
Kwa mujibu wa habari hizo, kocha huyo kutoka Bulgaria amewataka viongozi wa Yanga wahakikishe mchezaji huyo anatua nchini haraka iwezekanavyo, vinginevyo atagoma kumpokea.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa, kuchelewa kuwasili kwa mchezaji huyo kumevuruga programu ya Saintfiet, ambaye hadi sasa ameshindwa kupata kikosi cha kwanza cha kudumu.
Imeelezwa kuwa, awali kocha huyo aliwataka viongozi wa Yanga wahakikishe kuwa, Twite anakuja nchini pamoja na timu hiyo Jumatatu iliyopita, lakini mipango hiyo ilikwama baada ya mchezaji huyo kuomba ruhusa ya kwenda kuichukua familia yake Congo.
Kocha huyo pia ameulalamikia uongozi wa Yanga kwa kushindwa kumpatia usafiri wa uhakika na kumwacha aendelee kutumia basi dogo la klabu, ambalo anadai kuwa halifai kwa usalama wake.
No comments:
Post a Comment