KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 29, 2012

SERIKALI YABWAGWA KESI YA MINTANGA, MAHAKAMA KUU YAFUNGA USHAHIDI

Na Furaha Omary
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imeamua kufunga ushahidi wa upande wa Jamhuri katika kesi inayomkabili Rais wa zamani wa Shirikisho la Ngumi za Radhaa Tanzania (BFT), Alhaji Shaaban Mintanga, baada ya kushindwa kuleta mashahidi watano kutoka nchini Mauritius kwa muda mrefu.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Dk. Fauz Twaib anayesikiliza kesi hiyo, baada ya kukubaliana na ombi la jopo la mawakili waomtetea Alhaji Mintanga la kuiomba kufanya hivyo kwa mamlaka iliyokuwa nayo kwa mujibu wa sheria.
Alhaji Mintanga jana aliwakilishwa na mawakili Berious Nyasebwa, Aliko Mwamanenge na Jerome Msemwa huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Prosper Mwangamila na Wakili wa Serikali, Hamidu Mwanga.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Dk. Twaib alisema kwa muda wa vipindi vinne vya mahakama, upande wa Jamhuri umeshindwa kuleta mashahidi na kila mara umekuwa ukitoa hoja za kuomba kuahirishwa, ukosefu wa fedha, unafanya mawasiliano na kutumwa ofisa Mauritius na pia kwa vipindi hivyo umekuwa ukileta mawakili tofauti.
Jaji Dk. Twaib alisema alichobaini katika kesi hiyo ni ucheleweshwaji wa muda wa mahakama na kwamba Jamhuri walikuwa na muda mwingi wa kufanya yale waliyotaka kuyafanya.
Pia alisema kuna uzembe kwani upande wa Jamhuri kwa kupitia ofisi ya DPP ilikuwa inajua ilipaswa kumshauri Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kufuata taratibu za kumhoji mtu ambaye yupo nje.
"Kutokana na mazingira hayo, nimejiuliza mimi kama Jaji nitafanya nini, hivyo kwa mamlaka niliyopewa chini ya kifungu namba 264 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), ambayo inaongoza mwenendo wa mashauri ya jinai, ninaona ni vema kukubaliana na hoja za upande wa utetezi na kuamua kufunga ushahidi wa upande wa Jamhuri kwa kutoleta mashahidi kwa muda uliopangwa," alisema na kuutaka upande wa utetezi kuendelea na kesi kwa upande wao.
Awali, akianza kusoma uamuzi huo, Jaji Dk. Twaib alisema mshitakiwa Alhaji Mintanga anakabiliwa na mashitaka mawili ya kula njama na kusafirisha dawa za kulevya, ambayo amekana na upande wa Jamhuri ulitoa orodha ya mashahidi 29 ambao watano kati yao wapo nchini Mauritius.
Jaji huyo alisema Wakili wa Serikali Stella Machaku alifika mahakamani hapo na kueleza kuwa watatoa mashahidi tisa tu na kwamba wakati wa usikilizwaji, walitoa wanne na kubaki watano, ambao wapo nchini Mauritius.
Alisema kesi hiyo ilipangwa Februari, 2012 hata hivyo upande wa Jamhuri uliomba kuahirisha tena shauri hilo kwa kuwa hawana mashahidi na hivyo kupangwa Juni, 2011, ambapo tena waliomba ahirisho kwa madai Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) amewasiliana na maofisa wa serikali Mauritius kuona uwezekano wa kuwaleta mashahidi hao.
Pia alisema upande wa Jamhuri ulidai Mahakama Kuu haina fedha za kuwaleta mashahidi nao na kwamba ikishindikana watatoa ushahidi kwa njia ya video wakiwa Mauritius.
Jaji Dk. Twaib alisema shauri hilo lilipangwa Julai, mwaka huu, ambapo halikuendelea kwa kuwa alikuwa na majukumu mengine na hivyo kuahirishwa kwa takriban miezi miwili na nusu hadi Agosti 28, mwaka huu.
Alisema kesi hiyo ilipotajwa Agosti 28, mwaka huu, Wakili wa Serikali Mkuu, Arafa Msafiri akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Prosper Mwangamila waliomba kuahirishwa kwa shauri hilo kwa madai Agosti 23, mwaka huu, DPP alimtuma ofisa wake kwenda Mauritius.
Hata hivyo, mawakili wa utetezi walipinga ombi hilo kwa madai kama upande wa Jamhuri umeshindwa kuleta mashahidi hao, ambao watatu ni Watanzania (mabondia wanaodaiwa kukutwa na dawa hizo) na wawili ni raia wa Mauritius, basi ufunge ushahidi wao na pia mahakama itumie mamlaka iliyonayo kufunga ushahidi ili waendelee na kesi kwa upande wao.
Pia mawakili hao walidai sheria ipo wazi kwamba mahakama haiwezi kutoa uamuzi bila ya kuwepo kwa vielelezo vya nakala ya barua iliyopelekwa Mauritius na tiketi ya ofisa huyo aliyetumwa.
Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, Wakili wa utetezi Msemwa aliiomba mahakama wawasilishe hoja zao za kisheria iwapo wanaona mshitakiwa ana kesi ya kujibu au la.
Jaji Dk. Twaib aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 7, mwaka huu, ambapo upande wa Jamhuri na wa utetezi utawasilisha hoja hizo kabla ya mahakama kutoa uamuzi iwapo inaona Alhaji Mintanga ana kesi ya kujibu au la.
Mintanga anakabiliwa na mashitaka mawili ya kula njama na kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 4.8 kutoka nchini Tanzania kwenda nchini Mauritius. Dawa hizo zinadaiwa kuwa na thamani ya sh. milioni 120.

No comments:

Post a Comment