MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Ambwene Yesaya (AY) anatarajiwa kuondoka nchini mwezi ujao kwenda Marekani kwa ajili ya kurekodi video ya wimbo wake mpya.
AY, ambaye pia ni maarufu kwa jina la Mzee Biashara, atarekodi video hiyo na mwanamuziki Sean Kingstone wa Marekani.
Msanii huyo alipata bahati ya kurekodi na Sean Kingstone mwaka juzi wakati mwanamuziki huyo wa Marekani alipofanya ziara ya kimuziki nchini.
Wakati wa ziara hiyo, Sean Kingstone alisema yupo tayari kufanya kolabo na AY baada ya kuvutiwa na kipaji chake cha uimbaji.
“Natarajia kwenda Marekani mwezi ujao kufanya kolabo na tyga wa Cash Money, lakini pia nitatumia fursa hiyo kupiga picha za video ya wimbo wangu niliorekodi na Sean Kingstone,” alisema.
Kwa mujibu wa AY, amechelewa kurekodi video ya wimbo huo kutokana na Sean Kingstone kutingwa na kazi nyingi na hivyo kuwa bize.
AY alipata bahati ya kurekodi na Sean Kingstone bila malipo yoyote wakati wasanii wengine wamekuwa wakitozwa pesa nyingi. Jose Chameleone alitakiwa kulipa dola 30,000 za Marekani (sh. milioni 45) ili aweze kurekodi na mmarekani huyo.
“ Hizi kazi zinahitaji fedha nyingi, lazima uwe umejipanga kweli kweli, yaani ukienda, unafanya kazi, unamaliza unarudi zako,” alisema.
AY alisema alibahatika kurekodi nyimbo mbili na Kingstone na kuongeza kuwa, wimbo wa pili ndio atakaotengeneza video yake na mmarekani huyo.
Alisema kwa sasa hawezi kutaja jina la wimbo huo, lakini alidokeza kuwa, picha za video yake zitachukuliwa mjini Los Angeles, Marekani.
No comments:
Post a Comment