KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, August 14, 2012

BABA MZAZI AMZUIA MBUYI TWITE KUJIUNGA NA YANGA

Baba mzazi wa mwanasoka Mbuyi Twite amemzuia mwanaye kuja nchini kujiunga na klabu ya Yanga kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope alisema jana kuwa, wamepata taarifa kutoka Congo kwamba baba huyo, Mzee Twite anazitaka Simba na Yanga zikutane ili kumaliza utata uliojitokeza katika usajili wa mwanaye.

Mzee Twite ameelezea msimamo wake huo baada ya viongozi wa Simba na Yanga kuvutana kuhusu usajili wa mchezaji huyo wa APR ya Rwanda.

Awali iliripotiwa kuwa, Simba ilifanikiwa kumsajili mchezaji huyo kupitia Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage aliyekwenda Rwanda na kumsainisha mkataba, lakini baadaye zikaja taarifa kuwa, Yanga nayo imemsajili kupitia mjumbe wake wa kamati ya utendaji, Abdalla Bin Kleb.

Hans Pope ameilaumu Yanga kwa kuingilia kati usajili wa Twite na kuongeza kuwa, hali hiyo inaweza kuleta machafuko miongoni mwa mashabiki wa klabu hizo mbili.

Hans Pope amesema kitendo cha wenzao kuwazunguka na kumshawishi Twite kurejesha fedha walizompa ili asajili Yanga, kinaweza kuleta uhasama usio na ulazima.

"Tumepata taarifa kuwa baba mzazi wa Mbuyu (Twite) amemkataza mwanaye kuja kuichezea Yanga kwa hofu ya maisha yake.

"Mzee Twite anataka Simba na Yanga zikutane kufanya mazungumzo kwa lengo la kuweka mambo sawa kisha ndipo amruhusu kuja Tanzania," alisema Pope.

"Unadhani kwa kitendo walichofanya Yanga, mashabiki wa Simba watafurahi? Baba yake mzazi (Twite) amechukizwa na hali hiyo, anahofia usalama wa kijana wake," alisema Pope.

"Vita ya soka haina tofauti na ile ya siasa au dini. Kwa hiyo baba mzazi wa Mbuyu ameomba Yanga na Simba kumaliza suala hili mwanaye aweze kucheza soka kama ilivyo kazi yake.

"Katika kusisitiza ukweli wa madai yao, Pope alisema tayari uongozi wa Yanga umeomba kukutana nao ili kuzunguza na kumaliza suala hilo.

"Ukweli ni kwamba, hatuna tatizo na Yanga. Nafikiri siyo mara yao ya kwanza wala mwisho kutufanyia mchezo huu mchafu. Ni kawaida yao."

"Wameomba [Yanga] tukutane ili kumaliza utata wa suala hili, vinginevyo Twite hatakuja siyo kujiunga na Yanga au Simba, bali haji kabisa."

Aliongeza: "Tulianza mazungumzo na Bahanuzi (Said)wakatuzunguka na kumsainisha, ikawa hivyo tena kwa Kavumbagu (Didier) na sasa wametuma viongozi Kenya kutaka kumsainisha Pascal Ochien ambaye yupo na timu Arusha."

"Nafikiri Yanga kama wanataka kulipa kisasi cha mabao matano tuliyowafunga, wacheze mpira na siyo kutuzunguka na kusajili wachezaji wetu."

"Hata sisi tunaweza mchezo huo mchafu---ni kweli tunaweza kuwafanyia, lakini hatuoni sababu ya kufanya hivyo," alisema zaidi Pope.
Source: Mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment