KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 9, 2012

OKWI; SINA MPANGO NA YANGA

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda na klabu ya Simba, Emmanuel Okwi amesema hana mpango wa kujiunga na klabu ya Yanga.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam juzi, Okwi alisema hajawahi kukutana na kuzungumza na kiongozi yeyote wa Yanga kuhusu kujiunga na timu hiyo.
Okwi alisema bado yeye ni mchezaji wa Simba na hatarajii kujiunga na klabu nyingine ya Tanzania baada ya mkataba wake kumalizika kwa vile lengo lake ni kwenda kucheza soka ya kulipwa Ulaya.
Mshambuliaji huyo alisema amekuwa akipata taarifa zinazomuhusisha na mipango ya kujiunga na Yanga, lakini alisisitiza kwamba hazina ukweli wowote.
"Nauheshimu sana mkataba wangu na Simba na ninapenda kusisitiza kwamba siwezi kuzungumza na klabu nyingine kwa sasa kwa sababu sheria hainiruhusu,”alisema mshambuliaji huyo, aliyeifungia Simba mabao matatu wakati ilipoichapa Yanga bao 5-0 katika mechi ya mwisho ya ligi kuu msimu uliopita.
Alipoulizwa kuhusu matokeo ya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa aliyoyafanya katika klabu ya Red Bull Salzburg ya Austria, Okwi alisema alishindwa kumaliza kutokana na kuugua malaria. “Niliugua ugonjwa wa malaria na kusababisha nishindwe kufuzu majaribio hayo na kuamua kurejea nyumbani Uganda. Lakini viongozi wa klabu hiyo wamenieleza kwamba wataniita tena wakati wowote kwa ajili ya kuendelea na majaribio hayo,”alisema.
Okwi alisema mipango yake ya kufanya majaribio hayo haipo kwa klabu hiyo pekee kwa sababu wakala wake anaendelea kumtafutia nafasi katika klabu zingine za Ulaya.

No comments:

Post a Comment