LAGOS, Nigeria
WACHEZA filamu Segun Arinze na Justus Esiri wa Nigeria wiki iliyopita walikumbwa na mkasa baada ya kuporwa vitu vyao kadhaa kwenye hoteli moja mjini London, Uingereza.
Arinze na Esiri walikumbwa na mkasa huo wakati walipokuwa wamepanga kwenye hoteli ya Teavelodge iliyopo katika eneo la Surrey mjini London.
Kwa mujibu wa mtandao wa nigeriafilms, vyumba vya hoteli hiyo vina funguo tatu kila kimoja, moja ya mpangaji, ya meneja wa hoteli na nyingine ya mfanyakazi anayefanya usafi vyumbani.
Wacheza filamu hao walikuwepo London kwa mwezi mmoja katika ziara ya kuonyesha igizo la ‘The King must dance naked’ pamoja na maigizo mengine.
Imeelezwa kuwa, siku ya tukio, wacheza filamu hao walikuwa wamekwenda mazoezini na baada ya kurejea hotelini, waligundua kwamba vitu vyao vilikuwa vimepekuliwa.
“Baada ya kukagua mizigo yao, wakagundua kwamba baadhi ya vitu vyao vya thamani vimeibwa,” umeeleza mtandao huo.
Arinze aliripotiwa kupoteza Ipad wakati Justus alipoteza hati yake ya kusafiria, ikiwa na viza za kuingilia katika nchi kadhaa, nyaraka za safari, laptop pamoja na vitu vingine kadhaa vya thamani.
Kwa mujibu wa mtandao huo, tukio hilo liliripotiwa polisi, lakini hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na wizi huo. Pia imeelezwa kuwa, hoteli hiyo haikuwa na kamera za CCTV kwa ajili ya kurekodi matukio ya aina hiyo.
Kufuatia wizi huo, ubalozi wa Nigeria nchini Uingereza ulimpatia Justus hati mpya ya kusafiria.
Wacheza filamu wengine waliokuwepo kwenye ziara hiyo ni Olu Jacobs, Joke Silva na Bimbo Akintola na walitarajiwa kurejea nchini Nigeria jana.
No comments:
Post a Comment