KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, September 23, 2012

MINZIRO AMFUNIKA SAINTFIET


Hamisi Kiiza (kushoto) wa Yanga akigombea mpira na beki Ally Khan wa JKT Ruvu timu hizo zilipomenyana jana katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Yanga ilishinda 4-1. (Picha kwa hisani ya blogu ya kamanda wa matukio)

KAIMU kocha mkuu wa Yanga, Fred Felix Minziro jana alikianza vyema kibarua chake baada ya kuiongoza timu hiyo kuichapa JKT Ruvu mabao 4-1 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo ulikuwa wa kwanza kwa Yanga tangu ligi hiyo ilipoanza wiki mbili zilizopita. Katika mechi ya ufunguzi, Yanga ililazimishwa kutoka suluhu na Prisons mjini Mbeya kabla ya kupigwa mweleka wa mabao 3-0 na Mtibwa mjini Morogoro.
Yanga ililazimika kucheza mechi ya jana ikiwa chini ya Minziro baada ya uongozi kuamua kusitisha mkataba wa kocha Tom Saintfiet kutoka Ubelgiji kwa kosa la utovu wa nidhamu.
Mabao ya Yanga yalifungwa na Didier Kavumbagu, aliyefunga mawili, Nadir Haroub 'Cannavaro' na Simon Msuva. JKT ilipata bao lake la kufutia machozi kupitia kwa mkongwe Credo Mwaipopo.
Katika mechi zingine zilizochezwa jana, Azam iliichapa Mtibwa bao 1-0, Oljoro JKT iliichapa Polisi Morogoro bao 1-0 wakati Coastal Union ilitoka suluhu na Toto Africans.

No comments:

Post a Comment