KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, September 5, 2012

BAYSER: SIWANII UONGOZI TFF

MAKAMU wa pili wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Bayser amesema hana mpango wa kugombea nafasi yoyote ya uongozi katika uchaguzi mkuu ujao wa shirikisho.

Bayser amesema amekuwa akihusishwa na mipango ya kuwania urais wa TFF katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu, lakini ukweli ni kwamba hana mpango huo.

Mratibu huyo wa Mtibwa Sugar alielezea msimamo wake huo baada ya kutakiwa na Burudani aweke wazi iwapo ana mipango ya kuwania tena uongozi wa shirikisho hilo au la.

Bayser alisema binafsi anaamini kuwa wapo watu wengi wenye sifa na uwezo wa kushika nyadhifa mbali mbali za juu za uongozi wa shirikisho hilo.

"Mimi nipo na timu yangu ya Mtibwa Sugar,tunaendelea na maandalizi ya ligi kuu msimu ujao, sijapata wazo na wala sina mpango wa kutaka kuwania nafasi yoyote ndani ya TFF,"alisema Bayser.

Kiongozi huyo wa Mtibwa Sugar amewaomba wadau mbali mbali wa soka nchini wenye sifa na uwezo, kujitokeza kuwania nafasi za uongozi katika shirikisho hilo kwa lengo la kuendeleza mchezo huo.

"Nawaomba wadau walioko pembeni, ambao wameona mapungufu mbali mbali ya uongozi ndani ya TFF, wajitokeze kuwania uongozi pale muda utakapowadia,”alisema.

Mbali na Bayser, viongozi wengine wa zamani wanaotajwa kutaka kuwania tena uongozi ndani ya shirikisho hilo ni pamoja na aliyekuwa makamu wa kwanza wa rais, Crescentius Magori na katibu mkuu wa zamani, Fredrick Mwakalebela.

No comments:

Post a Comment