'
Thursday, September 13, 2012
AVEVA, BAKHRESA WAJITOSA DRFA
WAKATI uchaguzi mkuu wa Chama cha Soka cha Dar es Salaam (DRFA) umepangwa kufanyika Oktoba 14 mwaka huu, wanamichezo wengi maarufu nchini wamejitokeza kuwania nafasi mbali mbali za uongozi wa chama hicho.
Hata hivyo, mchuano mkali zaidi upo kwenye nafasi za mwenyekiti na katibu, ambapo baadhi ya wagombea waliojitokeza kuchukua fomu ni pamoja na mwenyekiti wa sasa, Amin Bakhresa na makamu mwenyekiti wa zamani wa Simba, Evans Aveva.
Bakhresa amekuwa kiongozi wa DRFA kwa miaka mingi, akiwa anabadilisha nafasi kutoka ya mwenyekiti kwenda ya ukatibu.
Hata hivyo, kuna habari kuwa Bakhresa anaweza kuwekewa pingamizi kutokana na kigezo cha elimu. Mwisho wa kupokea pingamizi kwa wagombea ni Septemba 20 mwaka huu.
Kujitokeza kwa wagombea hao, kumeifanya nafasi ya mwenyekiti kuwaniwa na wagombea watano hadi sasa.Wengine ni Salum Mkemi, Frank Mchaki na Jabir Juma.
Wagombea wengine waliojitokeza kuwania uongozi hadi sasa ni Salum Mwaking'inda na Gungulwa Tambaza ambao, wamechukua fomu za kuwania nafasi ya makamu mwenyekiti.
Waliochukua fomu za kuwania nafasi ya katibu mkuu ni Msanifu Kondo, Saidi Tuli na Hamisi Ambari,ambaye aliwahi kuwa meneja wa Yanga.
Wanaowania nafasi ya ujumbe wa mkutano mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni Amar Balhabou na Shafii Dauda wakati Benny Kisaka na Mohamed Bhinda wanawania uwakilishi wa klabu kwenye mkutano huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment