'
Saturday, September 29, 2012
MHOLANZI ARITHI MIKOBA YA SAINTFIET YANGA
Makamu mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga (kushoto) akiwa na kocha mkuu mpya wa timu hiyo, Ernstud Brandts.
KLABU ya Yanga leo imeingia mkataba na kocha mpya, Ernstud Brandts kutoka Uholanzi, ambaye amechukua nafasi ya kocha wa zamani, Tom Saintfiet kutoka Ubelgiji.
Brandts ameingia mkataba wa kuinoa Yanga kwa mwaka mmoja na kibarua chake cha kwanza kinatarajiwa kuanza kesho wakati timu hiyo itakapomenyana na African Lyon.
Mechi hiyo ya ligi kuu ya Tanzania Bara, inatarajiwa kuanza saa 11 jioni na itaonyeshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha SuperSport cha Afrika Kusini.
Brandts ametia saini mkataba huo mbele ya Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, Kaimu Katibu Mkuu, Lawrence Mwalusako na meneja mpya wa timu hiyo, Majid Saleh 'Kaburu'.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutia saini mkataba huo, Brandts alisema anafahamu wazi kuwa, jukumu alilokabidhiwa ni zito, lakini atajitahidi kadri ya uwezo wake kufanyakazi kwa bidii ili kuhakikisha Yanga inapata mafanikio.
Brandts alisema anaushukuru uongozi kwa kumuamini na kumpa kazi hiyo na kuongeza kuwa, cha muhimu ni kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi, wanachama na wachezaji.
Kabla ya kujiunga na Yanga, Brandts alikuwa kocha mkuu wa APR ya Rwanda, ambayo alikuja nayo nchini mwaka huu wakati wa michuano ya Kombe la Kagame.
Kwa upande wake, Sanga alisema wamepata kocha mjuzi na mwenye uzoefu mkubwa wa soka ya Afrika, hivyo wanaamini atawaletea mafanikio makubwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment